Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Lukuvi atoa miezi minne majengo, wapangaji NHC kufanyiwa uhakiki

86164 Pic+lukuvi VIDEO: Lukuvi atoa miezi minne majengo, wapangaji NHC kufanyiwa uhakiki

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameiagiza bodi na menejimenti ya Shirika la Nyumba, NHC ifikapo Machi 30, 2020 iwe na taarifa za wapangaji wote zilizohakikiwa.

Alisema pamoja na taarifa hizo kukamilika, bodi hiyo ihakiki upya taarifa za majengo wanayopangisha na waliyojenga.

Aliyasema hayo jana wakati alipokutana na bodi na menejimenti ya shirika hilo.

Waziri Lukuvi alisema wako watu wakihama kwenye nyumba hizo huziuza au kupangisha watu wengine kwa gharama kubwa. “Hakikisheni mnaanza utaratibu wa kidigitali kujua wapangaji wote ambao taarifa zao zitaendana na zilizo kwenye mfumo wa vitambulisho vya Taifa (Nida),” alisema Lukuvi.

“Wapo wanaomiliki nyumba zaidi ya moja kwa majina tofauti, ifikapo Machi 30 mwakani, daftari liwe limekamilika ili kubaini wapangaji hewa na wamiliki hewa,” alisema.

Waziri Lukuvi pia ameitaka bodi hiyo kwa kushirikiana na msajili, kuhakiki na kupitia upya majengo yote yaliyotaifishwa na serikali ambayo yameuzwa.

“Wapo waliopewa nyumba kwa masharti wakae hadi watakapofariki nyumba hizo zirudishwe serikalini lakini baadhi zimeuzwa na kubadilishwa umiliki,” alisema.

Pia, amelitaka shirika hilo hadi Januari mwakani kuhakikisha wamelipa kodi ya serikali shilingi 400 milioni na kukamilisha miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani.

“Muanze kutafuta vyanzo vya kupata fedha badala ya kukopa na kukamilisha miradi mliyoianza kwa fedha zenu wenyewe za ndani,” alisema.

Alisema nyumba zote za NHC zinazojengwa, zitajengwa na kampuni ya ujenzi ya shirika hilo na kuwataka hadi Desemba wawe wameanza kujenga majengo mengine kwenye kiwanja cha Dodoma.

Chanzo: mwananchi.co.tz