Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzalishaji wa mkonge ulivyoongezeka nchini

22827 Pic+mkonge Uzalishaji wa mkonge ulivyoongezeka nchini

Tue, 14 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imesema uzalishaji wa zao la mkonge nchini umepanda kutoka tani 19,700 mwaka 1970, hadi kufikia tani 36,000 mwaka 2019.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alisema uzalishaji huo kwa sasa hauridhishi ikilinganishwa na fursa zilizopo kwenye sekta ya mkonge.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa inafikia uzalishaji wa tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.

Mgumba, alisema kuwa lengo la serikali ni kujadili na kuzipatia majawabu changamoto katika zao la mkonge nchini, ili kuongeza tija katika uzalishaji, ajira na kukuza sekta ya viwanda, pato la mkulima na taifa kwa ujumla.

Alisema, pamoja na changamoto hizo, serikali inashughulikia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza tija na uzalishaji, kwa kuanzisha vitalu vya mbegu ya mkonge katika halmashauri zote ambako zao la mkonge linastawi.

Aidha, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano, uzalishaji wa mbegu bora umeanza ili kuzalishwa kwa wingi.

Pia alisema serikali inafanya uhakiki wa mashamba ya mkonge yaliyobinafsishwa ili yaweze kuzalisha, kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba, ikiwamo kutoa elimu kwa maofisa ugani katika vijiji na kata kwenye maeneo yanayolima zao hilo.

Alifafanua kuwa mambo mengine yanayofanywa na serikali ni kuongeza bajeti na kuwezesha kituo cha Utafiti Mlingano ili kufanya utafiti wa aina mbalimbali za mbegu ya mkonge na kuzisambaza kwa wakulima.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo, alisema kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza mnyororo wa thamani wa tasnia ya mkonge hususani kwenye viwanda na teknolojia bora za uzalishaji wa bidhaa za zao hilo.

Alisema mikakati ambayo serikali imeanza kuitekeleza na mafanikio yake yanahitaji ushiriki wa pamoja wa wadau wote wa tasnia ya mkonge.

Vile vile, Mgumba alisisitiza kuweka utaratibu na kukubaliana namna bora ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, utoaji wa elimu kwa wakulima na maofisa ugani.

Hata hivyo, alisema kuwa umefika wakati sasa wakulima kulima kilimo cha kisasa na cha kibiashara ili kuongeza uzalishaji na kuhimili ushindani wa soko la dunia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live