Imeelezwa kuwa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyoungwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia megawati 1,777.05 mwezi Desemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.87, ikilinganishwa na megawati 1,694.55 zilizokuwepo hadi kufikia mwezi Septemba 2022.
Aidha, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2022 jumla ya futi za ujazo milioni 38,172 za Gesi Asilia zilizalishwa katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay ambapo uzalishaji wa Gesi asilia umeongezeka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na kipindi Julai-Desemba, mwaka 2021 ambapo futi za ujazo 29,996 zilizalishwa.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ikiongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba ilipowasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati Taarifa ya Wizara kuhusu utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha mwezi Julai-Desemba, 2022.
Waziri wa Nishati, amesema kuwa, ongezeko la uwezo wa mitambo hiyo ya kuzalisha umeme iliyoungwa katika mfumo wa gridi limetokana kuingizwa katika Gridi ya Taifa megawati 90 za umeme zinazozalishwa katika Kituo cha Kinyerezi I Extension.
Aidha, amesema kuwa, uwezo wa kuzalisha umeme kwa mitambo ambayo haijaunganishwa katika Gridi ya Taifa umefikia megawati 39.302 na hivyo kufanya jumla ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kufikia megawati 1,816.352 ikilinganishwa na megawati 1,733.38 zilizokuwepo mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.89.
Kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji wa Gesi asilia amesema kuwa “ongezeko hili limetokana na ufungaji wa kompresa tatu katika Kitalu cha Songosongo ambazo zimeongeza mgandamizo na msukumo wa Gesi kutoka kisimani na sasa wastani wa futi za ujazo milioni 240 zinazalishwa kwa siku kutoka katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay.
Gesi hiyo inayozalishwa, inatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani, kwenye Taasisi, magari na uzalishaji wa wastani wa asilimia 62 ya umeme wa Gridi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati pamoja na kuishukuru Wizara kwa kuwasilisha utekelezaji wa Bajeti yake, alitoa maelekezo mbalimbali yatakayosaidia kutekeleza bajeti hiyo kwa ufanisi zaidi.
Katika kikao hicho na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wizara pia ilieleza utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ikiwemo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya Gesi na Umeme mijini na vijijini.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya Wizara.