Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzalishaji tumbaku nchini waongezeka

Tumbaku Malizano Uzalishaji tumbaku nchini waongezeka

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkakati wa Serikali kuingia ubia na sekta binafsi (PPP), unaonekana kuzaa matunda katika sekta ya ndogo ya tumbaku, ambapo mwaka 2022, uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kufikia tani 125 milioni, sawa na ongezeko la asilimia 92.3, ukilinganishwa na tani 65 milioni, zilizozalishwa mwaka 2021.

Hayo yamebainishwa Desemba 7, 2023 wilayani Morogoro na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (Torita), Dk Jacob Lisuma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchango wa taasisi hiyo kwenye zao hilo.

“Torita imetoa mchango mkubwa sana kwenye uzalishaji wa tumbaku nchini, ambapo mwaka jana tulizalisha mbegu bora zilizozalisha tani 125 milioni za zao hilo, tofauti na mwaka juzi ambapo uzalishaji ulikuwa tani 65 milioni tu.

“Ukifuatilia zao la tumbaku kabla ya kuanzishwa kwa Torita, uzalishaji ulikuwa chini ya tani 20 milioni, baada ya mwaka 2000 uzalishaji ulianza kupanda na kuwa tani 25 milioni, baadaye zikafika tani 65 milioni, na mwaka jana ndiyo zimefika tani 125 milioni, hivyo kuongeza kipato cha mkulima na Taifa kwa jumla,”amesema Dk Lisuma.

Amesema kuongezeka kwa uzalishaji huo kunatokana na mbegu bora walizozifanyia utafiti na kuzizalisha baada ya kutoridhishwa na uzalishaji mdogo uliokuwapo awali.

"Maelekezo Serikali yanaitaka Rorita kuwezesha uzalishaji wa tumbaku nchini, kufikia tani milioni 200 ifikapo mwaka 2025/2026. Ukiangalia bado tuna upungufu kidogo kufikia kiasi hicho ambacho tunaamini tutakifikia," amesema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Serikali imeamua kuwezekeza zaidi kwenye utafiti tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ambapo taasisi hiyo imepewa Sh500 milioni ambazo pamoja na mambo mengine zilizotumika kwenye uzalishaji wa mbegu bora na ununuzi wa vifaa vya maabara.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Torita, Profesa Gration Rwegasira amesema taasisi hiyo itahakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanatimia na hivyo kuleta tija katika uzalishaji wa tumbaku nchini.

“Torita imejikita katika kuzingatia mahitaji ya wakulima wakubwa na wadogo, vyama vya ushirika vya tumbaku, kampuni za ununuzi wa tumbaku na mifumo ya uendeshaji ya Serikali ili kuleta ufanisi na hivyo kuongeza pato la Taifa.

“Tunajivunia ushirikiano mkubwa uliopo kati yetu na wadau wa zao la tumbaku, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Bodi ya Tumbaku nchini ambapo kwa pamoja tumeweza kuimarisha uzalishaji wa zao hili na kuongeza tija,” amesema Profesa Rwegasira.

A mefafanua kuwa taasisi hiyo inazingatia uwepo wa Sua kama msingi mkuu wa kuhuisha utaalamu na teknolojia za kisasa kwa faida ya wakulima na Taifa kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live