Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzalishaji kahawa wazidi kudorora

Cofee Ed Uzalishaji kahawa wazidi kudorora

Fri, 18 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Kutokana na hali hiyo, serikali imewataka wadau wa zao hilo kutoa mapendekezo ya kuboresha ili kuongeza ufanisi kwenye uzalishaji wake.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akifungua kongamano la 11 la wadau wa kahawa kwa mwaka 2021.

Alisema uzalishaji wa kahawa mwenendo wake si mkubwa sana huku akitolea mfano wa mwaka juzi kuwa ulikuwa tani 68,000 wakati Uganda ulikuwa tani 400,000.

“Naamini kupitia kongamano hili, tutajadili kwa pamoja ili tuondokane na uzalishaji mdogo. Hata kule kwangu Songwe uzalishaji unashuka tofauti na ilivyokuwa awali.  Wakulima  wanahama kwenye uzalishaji, hivyo kupitia kongamano hili tutajua sababu ili tuje na mikakati ambayo itajibu maswali juu ya tatizo hili,” alisema.

Alitaja kero zingine zinazokabili sekta hiyo ndogo kuwa ni tija, uzalishaji mdogo, kuyumba kwa bei, ukosefu wa mitaji kwa wakulima na kutokopesheka kwenye taasisi za fedha, hivyo kuwafanya watu kuamini kuwa kilimo hakilipi.

Mgumba aliwataka wadau wa kahawa kutumia fursa hiyo kusikiliza kwa makini mawasilisho yatakayotolewa kwenye kongamano hilo na kutoa mapendekezo ya kuboresha zao hilo.

“Kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati ambayo yanatakiwa kubadilika na kukua na kutoa mchango wa serikali kwenye tatizo la ajira, kukuza uchumi na kuongeza kipato kwa wakulima,” alisema.

Mgumba alisema wadau hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha lengo la serikali linafikiwa na uzalishaji kahawa unabadilika kwa kuongeza ufanisi.

“Tuje na mbinu na mipango mipya itakayotoa ufumbuzi wa changamoto kuu zinazokabili zao la kahawa ikiwamo udumavu kwa uzalishaji wa kahawa,” alisema.

Mgumba alisisitiza kwamba sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na kwamba serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa sekta hiyo ili kufikia mapinduzi kwenye kilimo.

“Serikali imedhamiria kuleta mapinduzi kwenye kilimo na hatuwezi kusema tunaenda kwenye mapinduzi ya kilimo cha biashara bila sekta binafsi,” alisema.

Aliwahakikishia wadau kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta hiyo ili kufikia mageuzi kwenye kilimo huku akisema serikali itaendelea kuendeleza kilimo cha mkataba ili kulinda wawekezaji mitaji yao kwenye kilimo.

“Sekta binafsi tunawaona mara nyingi kwenye uzalishaji, serikali awamu ya sita itaheshimu kilimo hicho ili kuwavutia wawekezaji na si kuwachukulia kama madalali, kilimo kinahitaji fedha sasa yule anayewekeza ndio umdharau serikali ya awamu ya sita imesema haiwezi kufanya hilo,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Prof. Aurelia Kamuzora, alisema kongamano hilo watajadili sababu za baadhi ya wakulima wa kahawa kukimbilia kuuza Uganda ili kushauri serikali kuondoa vikwazo na kuleta tija kwenye uzalishaji wa zao hilo.

Chanzo: ippmedia.com