Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzalishaji kahawa wafikia tani 215,000

HASUNGA IPPMEDIA.webp Uzalishaji kahawa wafikia tani 215,000

Thu, 30 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema uzalishaji wa kahawa umeongezeka katika kipindi cha miaka minne hadi kufikia tani 214,962.

Hasunga alisema hayo jana jijini hapa wakati akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika uzalishaji wa zao hilo na kusema kwa wastani kila mwaka zimekuwa zikizalishwa tani 51,777 za kahawa nzuri, hivyo kuliwezesha taifa kuingiza fedha nyingi za ndani na za kigeni.

Pia alisema katika kipindi hicho, wakulima wamejipatia Sh. trilioni 1.195 ambazo zimewanufaisha kwa namna mbalimbali.

“Lakini kama taifa pia tumepata dola za Marekani milioni 427.9 ambazo ni fedha za kigeni katika kipindi hiki kitu ambacho ni mafanikio makubwa kwa wizara,” amesema.

Alifafanua kuwa kwa wastani baada ya kuanza kwa uandikishaji wa wakulima kwa lengo la kuwatambua ili kuwahudumia mpaka sasa wakulima 286,397 wamesajiliwa.

Alisema hao ndio wakulima wadogo ambao wanajishughulisha na zao hilo katika mikoa 16 na kwamba kuna wakulima wakubwa ambao wana mashamba 101 wanaozalisha kwa kiwango kikubwa.

Kuhusu ajira, alisema kahawa imechangia ongezeko la ajira za watu kutoka milioni 2.3 hadi milioni 2.7 ambao wamejiajiri au wameajiriwa kupitia kilimo cha kahawa na wanashiriki kwenye uzalishaji na mnyororo wa thamani.

Pia alisema mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa kwenye sekta ya viwanda limechangia kiwango viwanda takribani 554 ambavyo vinajishughulisha katika uchakataji kutoka katika ngazi ya uzalishaji mpaka ulaji.

Waziri Hasunga alisema viwanda hivyo viko katika madaraja tofauti, hivyo kuchukua nafasi hiyo kumpongeza Rais na viongozi wengine wakuu katika kuhamasisha uzalishaji, kuongeza tija, na uzalishaji wa zao hilo.

Sambamba na hilo, alisema uwekezaji umeongezeka katika utafiti ili kupata mbegu bora zinazofaa kwenye kilimo cha zao hilo, zinazotumia maji kidogo, zenye kustahimili ukame na zenye kukinzana na magonjwa ya kila namna.

Waziri Hasunga alieleza kuna aina nyingi za magonjwa yaliyokuwa yanalikabili zao hilo, lakini kwa sasa Taasisi ya Utafiti ya kilimo cha Kahawa (TaCRI) yenye ofisi katika kanda nane, utafiti ulikuja na mbegu 19 za kahawa aina ya Arabica ambayo inaonyesha mafanikio makubwa.

Alisisitiza kuwa pia kuna mbegu zingine tano aina ya Robusta ambazo zote kwa pamoja zinafanya kuwa na aina 23 za mbegu bora zilizofanyiwa utafiti wa kina na kutumika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live