Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekezaji zao la michikichi waongezeka

Mchikichi Uwekezaji zao la michikichi waongezeka

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KUTOKANA na kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta ya kula, serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wawekezaji, wakulima na Watanzania kwa ujumla kugeukia zao la michikichi kuongeza uzalishaji wa mafuta.

Licha ya Mkoa wa Kigoma hususani Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kuongoza kwa uzalishaji wa zao la michikichi nchini, uhamasishaji wa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika kilimo hicho umekuwa na changamoto nyingi kwani walikuwa wakitumia mbinu za mbao za matangazo kutangaza fursa hizo bila mafanikio.

Hata hivyo, baada ya kutumia tovuti zaidi ya wananchi 100 na kampuni 20 za sekta binafsi waliweza kujaza fomu ya kuomba kupata fursa katika kilimo cha uzalishaji michikichi.

Mafanikio hayo yamechangiwa na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma Awamu ya Pili (PS3+) unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti Ukimwi (PEPFAR), kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA).

Kwa pamoja zilifanyia maboresho na kutengeneza upya tovuti za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa nchi nzima kwa lengo la kusaidia ongezeko la upatikanaji wa habari na taarifa mbalimbali kwa wananchi na sekta binafsi.

Tovuti za mikoa na halmashauri zinasaidia wanachi na sekta binafsi kufahamu fursa za uwekezaji, taarifa za mapato na matumizi na fursa za ajira; kupata matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na sita kwa haraka na uhakika pindi majibu yatokapo na watumishi wa umma katika vituo vya afya na shule kupakua na kupakia taarifa za mishahara na kutuma fomu za maombi ya likizo bila kusafiri kwenda makao makuu ya halmashauri.

Hiyo imeokoa muda na gharama kwa watumishi ambao hapo zamani iliwapasa wasafiri mwendo mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kuchukua na kupeleka fomu za likizo makao makuu ya halmashauri zao. Akielezea mchango wa PS3+ katika kupata wawekezaji, Ofisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Winfrida Bwire anasema halmashauri hiyo inatumia tovuti kwa ajili ya kutoa matangazo ya kiutendaji, ikiwemo zabuni, ya ajira na fursa za uwekezaji.

Anasema mradi wa PS3+ ulitengeneza na kuboresha tovuti katika halmashauri na mikoa yote nchini, Uvinza ikiwa mojawapo. Aidha, aliendelea kusema zamani halmashauri hiyo walitumia kutangaza fursa kupitia mbao za matangazo, kupiga ngoma na kutangaza misikitini jambo ambalo lilifanya watu wengi kutofikiwa kwa wakati na kutofahamu fursa zilizopo.

Bwire anasema Machi, 2021 waliweka tangazo kwenye tovuti yao kuhusu uwekezaji wa michikichi na kupata matokeo makubwa kwani idadi ya watu wanaotembelea tovuti imeongezeka.

Kabla ya kuweka tangazo hilo, ni watu 15,000 pekee ndio walikuwa wanatembelea kwenye tovuti hiyo lakini kwa sasa zaidi ya watu 49,000 ndani na nje ya nchi wametembelea tovuti kupata taarifa za halmashauri.

Anasema kwa siku watu kati ya 100 hadi 150 hutembelea tovuti hiyo na wanapoweka matangazo ya fursa idadi ya watu huongezeka mara dufu. Bwire anaeleza baada ya tangazo hilo la uwekezaji wa zao la michikichi, watu wengi waliomba maeneo na idadi ya wawekezaji imeongezeka katika Wilaya ya Uvinza. Kwa mara ya pili, waliweka orodha kwenye tovuti hiyo kwa wale ambao walifanikiwa kupata mashamba na kwenda kukabidhiwa.

Mmoja ya mwekezaji ambaye amepata fursa ya uwekezaji kupitia tovuti, Anania Damas mkazi wa Kasulu Mjini, anasema tangazo la mradi huo aliliona kwenye makundi ya WhatsApp na lilielekeza kila anayetaka fursa hiyo, aingie kwenye tovuti.

Anasema alipolipata alimshirikisha rafiki yake ambaye yupo Kigoma lakini ana mashamba Uvinza ambapo alikiri kwamba tangazo hilo ameliona na amesikia kuhusu mradi wa michikichi. Anasema aliona kilimo cha michikichi ni sehemu sahihi ya kuwekeza; na kabla ya kuchukua hatua, aliamua kujiridhisha kwa kuingia kwenye tovuti ya halmashauri hiyo.

Fomu za maombi ya uwekezaji zilikuwa zinapatikana kwenye tovuti hivyo hakutumia gharama kufuata fomu badala yake alipakua moja kwa moja kutoka kwenye tovuti hiyo. Anasema faida za kutumia tovuti ni kufikia watu wengi kwa wakati mmoja kwani hakuna usiri badala yake huongeza uwazi na uwajibikaji.

“Tovuti ni njia nyepesi ya kuwafikia watu wengi tofauti na utangazaji wa kizamani. Uzuri wa tovuti

.unapata taarifa sahihi kwa sababu una uwezo wa kusoma mwenyewe taarifa, kujua vigezo na masharti tofauti na taarifa za kutumiwa,” anaongeza Damas.

Katika tovuti hiyo, tangazo la fursa ya uwekezaji katika michikichi lilieleza mwekezaji atasaidiwa kupata hati ya shamba lake jambo ambalo ni motisha na fursa kubwa kwa mwekezaji. “Nimezoea kulima kiholela, mashamba yangu yote hayana hati na katika vitu ambavyo vinatutesa Watanzania wengi ni kupata umiliki wa mashamba, tuna umiliki wa viwanja na nyumba lakini kwenye mashamba hatuna, niliona ni fursa ya kuwekeza,” anasema Damas.

Anasema kwa sasa amewekeza kiasi kidogo, lakini fursa hizo zikiendelea, atawekeza zaidi. “Nikipata umiliki wa shamba mimi ni mtu mwingine, itakuwa kama dhamana kwangu kwani nitakuwa na uwezo wa kukopa katika taasisi za fedha ili kuendeleza shamba,” anasema Damas.

Mhandisi Kilimo wa halmashauri hiyo, Salum Masolwa anasema mradi wa mchikichi ni wa kimkakati ambao unalenga kuongeza uzalishaji wa mafuta ndani ya wilaya na nchi kwa ujumla. Mradi huo pia unalenga kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

Baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa kulijumuisha zao la michikichi kwenye mazao ya kimkakati na kuzindua fursa za uwekezaji, waliandaa andiko kuhusu fursa hiyo. Anasema waliamua kujikita kwenye tovuti ili watu wanapopata taarifa kwenye vyombo vya habari, wawe na chanzo cha uhakika kinachotoa taarifa sahihi.

Anaeleza waliandaa tangazo hilo kwa ajili ya Watanzania na walio nje ya nchi na kuliweka kwenye tovuti. Masolwa anasema mtu aliyetaka fursa hiyo, alilazimika kutembelea tovuti ya halmashauri hiyo kupakua fomu; na kwamba tangazo hilo halikuwekwa kwenye mbao za matangazo kama walivyokuwa wanafanya zamani.

Mhandisi huyo anasema kwenye tovuti hakuna habari za uongo na sababu za kutofanikiwa katika masuala mbalimbali ni kutotumia tovuti. “Tulipoweka hili tangazo watu 184 waliomba ndani ya muda mfupi na kilichowavuta tangazo lilizunguka sana na kuunganishwa na tovuti. Mwanzoni matumizi ya tovuti yalikuwa si sana lakini sasa kila wakati halmashauri inatoa taarifa kwenye tovuti ambazo zinaunganishwa na mitandao ya kijamii,” anasema. Mradi huo umegawanyika katika makundi mawili; wawekezaji wadogowadogo ambapo mkulima mmoja ana ekari tano hadi 25 lakini pia wana mwekezaji mkubwa ambaye aliomba ekari 500 na wakampatia.

Anaeleza mwekezaji huyo pamoja na kulima michikichi ana matarajio ya kuwa na kiwanda cha kuchakata mafuta na mazao mengine yatokanayo na zao hilo. “Eneo hili ni la ekari 800 kati ya hizo ekari 402 zimeshaandaliwa na wakulima wenyewe.

Utaratibu wa malipo kwa shamba hili; gharama ya fomu ni Sh 20,000 na itatakiwa kujazwa na kutumwa kwenye email ambayo ipo kwenye tangazo. Waliofanikiwa walijulishwa kupitia tangazo lililowekwa kwenye tovuti sambamba na kujulishwa wamepata fursa hiyo pamoja na bili zao.”

Wanalenga pia kuweka miundombinu ya umwagiliaji ambayo itasimamiwa na chama cha ushirika. Masolwa anasema: “Kilimo hiki tunakitegemea kuwa chanzo kizuri cha mapato kwa baadaye kwani mpaka kuvuna inachukua miaka mitatu. Kama serikali tumewekeza na lengo letu ni kupata mapato yanayotokana na mazao haya.

Mweka hazina wa Halmashauri ya Uvinza, Majidi Mabanga anasema halmashauri hiyo imekuwa na mikakati ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato kwani ndio kipaumbele cha serikali. Anasema baada ya tangazo hilo, takribani watu 184 waliomba kupatiwa mashamba na baada ya mchakato wa kulipia, mashamba 59 yamegawiwa kwa wawekezaji.

“Kupitia tovuti yetu tulipata mwekezaji mmoja kutoka nchini Burundi ambaye amechukua ekari 200 na watu wanaendelea kuomba hivyo utaongeza mapato katika halmashauri yetu na mchango huu umechangiwa na Mradi wa PS3+ kwa kuboresha tovuti yetu na kuhakikisha upatikanaji wa habari kwa wakati,” anasema Mabanga.

Anasema gharama zote za kuandaa shamba, kumkabidhi mmiliki pamoja na hati yake kwa ekari moja ni Sh milioni 3.8. “Kwa gharama hiyo halmashauri inasafisha shamba la mwekezaji, inapanda michikichi na kumpatia hati na mkakati huo unaendelea.”

Anasema ni matumaini yao baada ya miaka mitatu ya kuanza kuvuna zao hilo, kipato cha Halmashauri ya Uvinza kitaongezeka mara dufu. Lengo la PS3+ ni kuimarisha mifumo ya sekta za umma kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na uwajibikaji kwa wananchi, hivyo kupitia tovuti waliyoiboresha, imefanikiwa kuiwezesha Halmashauri ya Uvinza kuongeza vyanzo na ukusanyaji wa mapato. Mabanga anasema fedha hizo kutokana na mashamba watatekeleza miradi kwa kutumia mapato ya ndani katika ujenzi wa shule, vituo vya afya na zahanati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live