Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari nchini Kenneth Bengesi amesema juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali zimepunguza matumizi ya fedha za kigeni ya kuagiza sukari nje ya nchi kutoka dola zaidi ya million 300 hadi dola milioni 140 mpaka 150, zinazotumika hivi sasa kwa shughuli hiyo.
Akizungumza na waandihsi wa Habari kwenye banda la Bodi hiyo katika Viwanja vya John Mwakangale, Bengesi amesema, juhudi hizo zitaleta ukombizi mkubwa katika uchumi wa wananchi na Taifa.
Amesema, “tunapoagiza sukari nje ya nchi tunatumia fedha nyingi za kigeni , na sasa hivi pamoja na kwamba tumepunguza kiasi cha sukari kutoka nje lakini bado tunatumia takribani dola milioni 140 hadi dola milioni 150 kwa ajili ya kuagiza sukari kwa mwaka ,kiasi hicho ni kikubwa ambacho kingeweza kutumika kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii.”
Hata hivyo, amesema kutokana na uwekezaji mkubwa na upanuzi wa viwanda vya Sukari Serikali inatarajia kuongeza uzalishaji wa sukari huku lengo likiwa ni kuzalisha kiasi cha kutosheleza mahitaji ya ndani na ziada kuuzwa nje ya nchi. “Kwa mara ya kwanza uwekezaji mkubwa sana umefanyika katika tasnia ya sukari na uwekezaji huu umefanyika katika viwanda vilivyokuwepo kwa maana upanuzi mkubwa sana umefanyika utaona unaendelea kwa mfano ukienda Kilombero kuna kiwanda Kipya Cha K4 kinachojengwa ambapo chenyewe peke yake kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa sukari wa tani 144,000 ukijumlisha na hiki kilichopo sasa hivi kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 271,000 ifikapo mwaka 2025.” amefafanua Bengesi. Ameongeza kuwa, “Kagera sugar napo kuna upanuzi mkubwa wa mifumo ya umwagiliaji,kwenye mashamba na kwenyewe upanuzi mkubwa umefanyika na hiyo yote inakwenda kuongeza uzalisha wa sukari kutoka tani 124,000 za sasa mpaka tani 170,000 ifikapo mwaka 2025 na kule Mtibwa nako kuna mabwawa mengi yanajengwa.