Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekezaji waongezeka, miradi 293 yasajiliwa

Mwigulu Miradi Uwekezaji waongezeka, miradi 293 yasajiliwa

Thu, 15 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imepiga hatua katika uendelezaji wa sekta binafsi huku kukiwa na ongezeko la asilimia 14.5 ya usajili wa miradi mipya ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani 4,537.7 milioni.

Ongezeko hilo linaloelezwa linachangiwa na juhudi za Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, amesema hayo leo Alhamisi Juni 15, 2023 alipowasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa katika mwaka 2022.

Amesema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa mwaka 2022 kimesajili miradi 293 ikilinganishwa na 256 iliyosajiliwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.5.

Kati ya hiyo, miradi 99 ilikuwa ya Watanzania, huku 112 ikiwa ni ya wageni na miradi 82 ni ubia kati ya Watanzania na wageni.

Waziri Nchemba amesema thamani ya miradi iliyosajiliwa ilikuwa Dola za Marekani 4,537.7 milioni mwaka 2022 ikilinganishwa na Dola 3,749.3 milioni za mwaka 2021.

“Ongezeko la thamani na idadi ya miradi iliyosajiliwa lilichangiwa na juhudi za Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji,” anasema Dk Mwigulu.

Amesema miradi iliyosajiliwa ilikuwa na fursa za ajira 40,889 mwaka 2022 ikilinganishwa na 53,025 mwaka 2021.

Akizungumzia mgawanyiko wa usajili wa miradi kisekta kwa mwaka 2022, amesema sekta ya uzalishaji viwandani iliongoza kwa kusajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani 3,277.0 milioni ikifuatiwa na ya usafirishaji Dola 647.7 milioni na ya ujenzi wamajengo ya biashara Dola 184.2 milioni.

“Katika kipindi hicho, sekta iliyosajili idadi kubwa ya miradi ilikuwa uzalishaji viwandani ikiwa na miradi 141, ikifuatia usafirishaji mizigo miradi 58 na kilimo miradi 29,” amesema.

Dk Mwigulu akizungumzia mgawanyiko wa miradi kimkoa kwa mwaka 2022, amesema Dar es Salaam uliongoza kwa kuvutia miradi ya uwekezaji kwa asilimia 42.3 ikifuatiwa na Pwani (asilimia 15.0), Arusha na Mwanza (asilimia 5.5) kila moja na Dodoma (asilimia 4.1).

“Hii ilitokana na uwepo wa mazingira wezeshi ya uwekezaji, hususan miundombinu bora,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live