KAMPUNI za madini nchini zimetakiwa kuboresha huduma za jamii kwenye vijiji vinavyozunguka migodi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, maji, vituo vya afya na shule.
Hiyo ni sehemu ya mikakati ya utekelezaji wa Dira ya Madini ya 2030 iliyoainishwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba leo jijini Dar es Salaam ambapo imejipambanua kwa moto wa 'Madini ni Maisha na Utajiri'.
Mhandisi Samamba amesema Tume ya Madini imejipanga kuboresha usimamizi wa Sekta ya Madini. Katika kutekeleza hayo imejikita katika kuwainua wachimbaji wadogo nchini kwa kuendelea kutenga maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kijiolojia kwa wachimbaji wadogo ili uchimbaji wao uweze kuwa na tija pamoja na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa watanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini nchini.
Amesema kuwa utekelezaji wa Dira hii katika Sekta ya Madini inawalenga zaidi wachimbaji wadogo wa madini ambao wamekuwa wakiwekeza lakini manufaa yamekuwa si ya kuridhisha kutokana na kutokuwa na taarifa za kutosha za utafiti za madini na teknolojia duni kwenye uchimbaji wa madini.
Amefafanua kuwa Tume itaendelea kuimarisha usimamizi katika shughuli za madini kwa kutenga maeneo yenye taarifa za kijiolojia yaliyofanyiwa tafiti ili kuweza kunufaika na rasilimali hizo sambamba na kuandaa Mpango Kazi utakaolenga kusimamia maeneo ya elimu za ugani; kuboresha mfumo wa utoaji wa leseni; ukaguzi migodi na mazingira; usimamizi wa masuala ya afya na usalama mahala pa kazi pamoja na kuimarisha mifumo ya makusanyo ya maduhuli.
Mhandisi Samamba amesema katika kutekeleza dira ya madini ya 2030, Tume imejikita katika kutoa elimu kwa wamiliki wote wa migodi kuhusu kutoa kipaumbele kwa huduma na bidhaa zote zinazotolewa na watanzania pamoja na kuandaa namna bora ya kuingia ubia kati ya kampuni za watanzania na kampuni za nje na uwepo wa utekelezaji wa Sheria ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini pamoja na Urejeshaji wa Huduma kwa Jamii. -