Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekezaji nchini wapaa hadi trilioni 21.3

2bbb84bbc0b6260b317bd13b33c0ed88.jpeg Uwekezaji nchini wapaa hadi trilioni 21.3

Wed, 29 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kipindi cha mwaka mmoja Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imezidi kufanya vizuri kiuchumi kwa kuongeza uwekezaji hadi kufi kia dola za Marekani bilioni 9.2 sawa na Sh trilioni 21.3 kutoka chini ya dola za Marekani bilioni moja.

Aidha, mauzo ya nje katika kipindi hicho pia yameongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 10 sawa na Sh trilioni 23.1 kutoka dola za Marekani bilioni saba hadi nane.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Profesa Godius Kahyarara alipozungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ulioandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kuhusu mafanikio ya ziara ya siku tatu ya Rais Samia nchini Oman hivi karibuni.

“Haya yote ni matokeo chanya ya filamu ya Royal Tour, ziara za Rais nje ya nchi na jitihada nyingine za serikali. Kufikia hatua hii ni jambo la kushangilia kwetu kwa sababu kupitia Royal Tour faida kubwa tutakayoipata kwa kuongeza watalii itatusaidia sana kuongeza zaidi mauzo nje,” alieleza Profesa Kahyarara.

Alisema maono ya serikali hadi ifikapo mwaka 2025 mauzo ya bidhaa nje ya nchi yanatakiwa yafikie angalau asilimia 30 ya Pato la Taifa (GDP), hali ambayo alieleza kuwa inaweza kufikiwa kutokana na kasi ya mauzo ilivyo nje ya nchi.

“Sasa hii maana yake nini, yatatusaidia kutuletea ahueni kwenye deni la taifa, tukiongeza mauzo nje tunapunguza makali ya deni la Taifa,” alisema.

Alisema mafanikio hayo yamefanyiwa tathmini kuanzia Machi, mwaka jana hadi Juni 25, mwaka huu. Alieleza kuwa mafanikio hayo makubwa yataipandisha Tanzania kiuchumi ndani ya jumuiya na Bara la Afrika.

Royal Tour:

Katibu Mkuu huyo alisema baada ya kuzinduliwa kwa filamu hiyo, kwa sasa watalii na wawekezaji katika sekta ya utalii wameongezeka ambako kwa mujibu wa hoteli za kitalii Dar es Salaam, ongezeko la wageni limefikia asilimia 280 na Arusha asilimia 340.

Alisema kwa upande wa viwanja vya ndege, miruko ya ndege imeongezeka ikiwamo ndege zinazoingia nchini. Alieleza kuwa ikilinganishwa na kipindi cha kabla, baada ya janga la Covid-19 na baada ya Royal Tour mashirika ya ndege nyingi za kimataifa yameanza kupeleka ndege zao nchini.

Alitolea mfano kuanzia Juni mwaka jana hadi Juni 25, mwaka huu, mashirika makubwa ya ndege yameongeza safari zake nchini kama vile Fly Dubai ilikuwa na ndege 10 sasa zipo 14, Oman Air zilikuwa ndege mbili sasa zipo saba kwa wiki, Kenya Airways zilikuwa 19 sasa 22, Emirates zilikuwa nne sasa saba kwa wiki na Turkish Air zilikuwa nne sasa saba kwa wiki.

“Kwa wastani ongezeko la safari hizo za ndege ni kutoka 93 mpaka 124 kwa wiki,” alisema Profesa Kahyarara. Uwekezaji Kuhusu uwekezaji nchini alisema umeongezeka kwa kiasi kikubwa hususani wawekezaji kutoka Marekani ambao kuna mwekezaji mmoja kutoka Marekani anayetaka kuwekeza kwa kujenga hoteli za kisasa za kitalii katika maeneo sita ambayo ni Serengeti, Ngorongoro, Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es Salaam.

Alisema tayari mwekezaji huyo ameshafika katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambako ameahidi hadi kufikia mwaka 2024 atakuwa amekamilisha ujenzi wa hoteli hizo.

“Lakini pia serikali imejipanga kufufua hoteli zote zilizokufa na tayari Hoteli ya Southern Sun itafunguliwa na Double Tree itafunguliwa lakini kwa jina la Delta Marriot ambayo ni brand ya Marekani na brand nyingi tu zinakuja. Huu ni msukumo wa Royal Tour,” alisema.

Mifugo:

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema serikali imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti milipuko ya magonjwa katika mifugo ili kukidhi vigezo vya kuuza nyama kimataifa.

Alitaja moja ya mikakati hiyo kuwa ni kuanza utambuzi na usajili wa mifugo yote nchini kwa njia ya elektroniki, kila kijiji kuwa na josho la kuogeshea ng’ombe pamoja na kila mfugo kupatiwa dawa kitaalamu.

Alielezea kuridhishwa na masoko ya nyama kuanza kufunguka ikiwamo kuondolewa kwa zuio la kuingiza nyama Saudi Arabia kutoka Tanzania hali ambayo sasa itasaidia viwanda vinne vilivyo nchini vya kuchakata nyama kufanya kazi kwa uwezo wake.

“Viwanda hivi vilikuwa vinachakata nyama chini ya uwezo wake yaani asilimia 20 hadi 30 tu ya uwezo wake kutokana na soko. Lakini sasa nchi inafunguka tutatafuta masoko kwa hali na mali kwa kuwa Tanzania ina mifugo mingi,” alisema Ndaki.

“Hivyo tumejipanga kudhibiti hali ya magonjwa na kukidhi vigezo vya kuuza nyama katika nchi za Saudia na Oman. Kwa sasa tuna uwezo wa kusajili na kutambua mifugo yote kwa njia ya elektroniki,” alieleza Ndaki.

Alisema katika kufanikisha hilo, wameanza mchakato wa kutambua na kusajili mifugo, na tayari ng’ombe milioni tatu wametambuliwa na kusajiliwa kazi itakayokamilika Septemba, mwaka huu. Usafirishaji ngozi Ndaki alikiri kuwa ngozi zinazozalishwa nchini asilimia 98 hazina ubora, hali inayosababisha kutokidhi vigezo katika soko la dunia.

Alisema wafugaji wengi wamekuwa wakitumia mbinu ya kupiga chapa mifugo hali inayosababisha kupunguza ubora wa ngozi na kukataliwa kimataifa.

Alisema katika kutatua tatizo hilo serikali imeanza kutoa elimu kwa wafugaji, kuanza kutumia mbinu ya kisasa ya utambuzi wa mifugo kwa kuwavalisha hereni mifugo.

Ziara Oman:

Awali, akizungumzia kwa ufupi ziara ya Rais Samia nchini Oman, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus alisema ziara hiyo imezaa matunda mengi ikiwamo makubaliano ya nchi hizo mbili katika sekta za biashara na uchumi na kudumisha uhusiano wa kirafiki uliopo wa muda mrefu.

Alisema pia ilisainiwa mikataba saba ya ushirikiano baina ya serikali na taasisi za serikali inayogusa sekta kama vile nishati, utalii, mifugo, biashara na uwekezaji.

Nishati Waziri wa Nishati, January Makamba alielezea namna wizara yake ilivyojipanga kuboresha upatikanaji wa umeme nchini hususani wakati huu wa ongezeko la uwekezaji na kubainisha kuwa takribani Sh trilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu.

“Tunao uwezo wa kutosha wa kupata umeme kwa ajili ya uwekezaji nchini. Na hata sasa mahitaji ya umeme makubwa kabisa kuwahi kurekodiwa yamefikiwa mara nne tu na ni megawati 1,336 wakati uwezo wa uzalishaji ni megawati 1,600,” alisema January.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live