Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekezaji mpya Bandari ya Dar

Uwekezajipoiic Data Bandari Uwekezaji mpya Bandari ya Dar

Sun, 7 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ziara za Rais Samia Suluhu Hassan katika mataifa zaidi ya 10 duniani zimeonyesha uhalisia katika maisha ya Watanzania kupitia kasi ya ongezeko la watalii, mtandao wa biashara na mikataba ya uwekezaji unaoonekana kwa tathmini ya miezi mitano.

Miongoni mwa matokeo hayo ni tukio la juzi baada ya kampuni mbili za kimataifa kusaini mkataba wa makubaliano ya awali (MOU), utakaoifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za bandari Afrika Mashariki, ikiwa ni matokeo ya ziara yake katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Makubaliano hayo yanafanyika ikiwa ni miezi mitano imepita tangu Rais Samia alipofanya ziara hiyo alikofanikisha utiaji saini wa hati za MoU 36 zenye thamani ya Sh17 trilioni na mikopo ya riba nafuu.

Kampuni ya AD Ports Group ilisaini mkataba huo na kampuni ya Adani na SEZ Ltd kwa ajili ya uwekezaji wa pamoja wa kimkakati unaohusisha reli, huduma za baharini, uendeshaji wa bandari, huduma za kidijitali, eneo la ukanda wa viwanda na uanzishaji wa vyuo vya elimu ya baharini hapa nchini.

Mkurugenzi mtendaji na mtendaji mkuu wa AD Ports Group, Kapteni Mohamed Juma Al Shamisi alinukuliwa katika taarifa yake akisema mkataba huo pamoja na kuifanya Tanzania kitovu, utawezesha pia kupanua mtandao wa kimataifa wa kampuni hizo kupitia kasi na ufanisi wa kufika katika masoko.

Matokeo mengine ya ziara hizo ni ugeni wa wawekezaji waliokuja nchini wiki nne zilizopita, baada ya Rais Samia kumaliza ziara nchini Omani, wakiwa na uhitaji wa ekari 10,000 za uwekezaji wa kilimo cha mazao mbalimbali kama ilivyoelezwa na Judica Omary, ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Mbunge wa Afrika Mashariki, Fancy Nkuhi aliyepokea wawekezaji hao mkoani alisema tayari wameonyesha dhamira ya kuwekeza, hususan kilimo cha parachichi.

Matokeo mengine ni tukio la Juni 11, mwaka huu baada ya Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kusaini marekebisho ya itifaki katika mkataba wa huduma za usafiri wa anga kati ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa wizara ya uchukuzi, mkataba huo unahalalisha mashirika yenye ndege kubwa kati ya Tanzania na Marekani kuanza safari kutoka na kuingia ndani ya majiji ya nchi hizo, ikiwa ni utekelezaji wa matokeo ya ziara ya Rais Samia nchini Marekani Aprili 14 hadi 26, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live