MKURUGENZI wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka Sh trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia Sh trilioni 76 mwaka 2023 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 8.6.
Akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Matinyi amesema, sababu ya ongezeko hili ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.
“Ofisi imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka shilingi bilioni 637.66 hadi trilioni 1.008 kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 58,” amesema kiongozi huyo.
Amesema, serikali pia imeongeza umiliki wa hisa katika kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka asilimia 25 hadi asilimia 37 huku ikisaini mikataba ya ubia wa asilimia 16 zisizohamishika katika kampuni za madini.