Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekezaji kufunguka zaid Tanzania

4c15367e60419ecda716f99301923130 Uwekezaji kufunguka zaid Tanzania

Mon, 25 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais, Samia Suluhu Hassan amesema makala maalamu ya televisheni ya The Royal Tour itaongeza fursa za ajira nchini.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia ameeleza kuwa makala hayo yanakusudia kutangaza na kukuza sekta ya utalii nchini.

“Aprili 18 nimeshiriki katika uzinduzi wa makala maalumu iitwayo ‘Tanzania: The Royal Tour’ nchini Marekani. Makala hii inakusudia kutangaza na kukuza sekta yetu ya utalii katika soko la kimataifa na kuongeza fursa zaidi za ajira zitokanazo na utalii na uwekezaji nchini,” aliandika.

Rais Samia alieleza kuwa wakati akiwa katika ziara yake nchini Marekani alikutana na kuzungumza na wawekezaji kwenye sekta za madini, nishati, afya na teknolojia.

“Mazungumzo haya ni hatua muhimu katika kufungua fursa zaidi za uwekezaji kwa nchi yetu na uboreshaji katika sekta hizi,” aliandika.

Alieleza kwa sasa kuna idadi kubwa ya Watanzania wengi wao wakiwa vijana waliojiajiri kupitia sanaa hasa muziki na filamu.

“Nikiwa nchini Marekani nilitenga pia wasaa kujadiliana na wadau wakubwa wa sekta hii nchini humo ili kupanua wigo kwa Watanzania walio katika sekta hii kunufaika kimataifa,” aliandika.

Askofu William Mwamalanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashehe ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini akizungumzia filamu hiyo alimpongeza Rais Samia kwa kuwa Rais mwanamke wa kwanza duniani kutengeneza filamu hiyo.

Aliwashauri vijana wasomi waitumie filamu hiyo kwa lengo la kupata fursa za kibiashara zilizomo ndani yake.

Rais Samia alishiriki katika uzinduzi wa filamu hiyo uliofanyika New York na Los Angeles, Marekani wiki iliyopita na kukutanisha watu mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali.

Akihojiwa wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania ni sehemu bora kwa kutembelea na kuwekeza kutokana na kuwa Watanzania ni watu wakarimu, wenye upendo na marafiki.

“Kitu ambacho watu hawakijui na wanaweza kuvutiwa zaidi na Tanzania ni kwamba ni nchi yenye watu wenye upendo, wakarimu na marafiki. Mtu yeyote akija Tanzania hata kwa bahati mbaya nakuhakikishia kamwe hawezi kujutia,” alisema.

Muongozaji na Mhariri wa filamu hiyo, Peter Greenburg alieleza namna ilivyorekodiwa na kwamba walitumia muda wa saa 14 hadi 15 kwa siku katika kuitengeneza.

Alisema walikuwa wakiamka saa 11.00 alfajiri na kulala saa 4:00 hadi 5:00 usiku.

Alisema baada ya uzinduzi wa filamu hyo nchini Marekani, itaoneshwa sehemu mbalimbali nchini humo kwa zaidi ya miezi mitatu na kuanzia Ijumaa iliyopita ingepatikana pia katika televisheni za Amazon Prime na Apple Tv Plus.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live