Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekezaji bandari ya Tanga kuongeza mapato

Tanga Ports Ath.jpeg Maboresho ya bandari ya Tanga yakiendelea

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika bandari ya Tanga kwa kuongeza kina cha maji, utaisaidia kuongeza mapato na kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea bandari hiyo jana, wadau wanaohudhuria mkutano unaojadili changamoto zinazoikumba bandari ya Dar es salaam, walisema upanuzi wa gati katika bandari ya Tanga utasababisha waweze kuhudumia meli kubwa.

Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Wakala wa Meli nchini (TASAA) Daniel Malango alisema mabadiliko yaliyofanyika yanaleta suluhisho la meli zilizokuwa zikishushia mizigo nchi jirani ya Kenya, zitafika katika bandari hiyo.

"Tulichokiona Tanga tunaweza kusema ni 'game changer' kwamba kuna uwekezaji serikali imefanya, sasa naiona Tanga inakuwa suluhisho la mizigo iliyokuwa inapitia bandari ya Mombasa, Meli kubwa zitafika hapa na Revenue zetu zitakuwa juu," alisema Malango.

Alisema matayarisho yaliyofanywa kwa ajili ya kontena na mizigo mingine itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa mapato yatapanda, lakini pia wasafirishaji watatumia muda mfupi zaidi.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka alisema mradi wa maboresho ya bandari katika kuhudumia mizigo kutoka tani laki saba hadi kufikia tani milioni tatu unaofanywa katika bandari hiyo utasaidia kufikia kina cha mita 13 utasaidia meli kubwa kuweka gati bandarini.

Alisema mradi huo ukikamilika utasaidia kupunguza mizigo inayohudumiwa katika bandari ya Dar es salaam hasa kwa wakazi wa mikoa ya Kaskazini na kwasasa watatumia muda mfupi kupitia bandari ya Tanga.

Awali meneja wa bandari ya Tanga, mhandisi Masoud Mrisha alisema mradi huo ambao upo awamu ya pili ya utekelezwaji wake umefikia asilimia 45 na unatarajiwa kukabidhiwa Novemba mwaka huu utakaokuwa na mita 450.

Alisema mradi huo ukikamilika utaweza kuhudumia kiasi cha tani milioni 3 ambapo kwa sasa bandari hiyo inauwezo wa kuhudumia shehena ya tani laki saba tu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live