Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekaji vinasaba mafuta petroli unavyookoa mamilioni

43ed5e0ecb8154e2b13c5446cf6cd2be Uwekaji vinasaba mafuta petroli unavyookoa mamilioni

Tue, 6 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KWA muda mrefu sasa, wauzaji wa nishati ya mafuta ya petroli na dizeli nchini wamekuwa wakituhumiwa kudanganya kwa kuchanganya nishati hiyo kwa lengo la kujipatia faida zaidi katika mauzo.

Kwa kutambua hilo, Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA) imekuwa ikifuatilia wafanyabiashara wanaodanganya kwa kuchakachua mafuta hayo kwa lengo la kudhibiti uhalifu huo.

Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titusa Kaguo anasema, serikali imechukua hatua kali kukomesha uhalifu huo kwa kuanzisha mradi wa kuweka vinasaba kwenye mafuta yanayosambazwa hapa nchini.

Anasema, Desemba 2006, Serikali ilianza kudhibiti Sekta Ndogo ya Mafuta kupitia EWURA ambapo wakati huo, sekta hiyo ilibainika kuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uchakachuaji wa mafuta (fuel adulteration) na kuingiza kwenye soko (dumping) mafuta ambayo hayalipiwi kodi yanayopita nchini kwenda nchi jirani, mafuta ya magendo kutoka nchi jirani na mafuta yaliyosamehewa kodi kwa ajili ya miradi maalumu ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Kaguo, changamoto hizi zilikuwa zinasababishwa na wafanyabiashara wasio waaminifu, ukosefu wa nyenzo na taratibu za kudhibiti changamoto hizo. Hali hiyo ilisababisha mafuta yenye ubora hafifu kuwepo kwenye soko, kuharibu ushindani na kuikoshesha Serikali mapato ya kodi inayotokana na uuzaji wake.

Anasema, mwaka 2007, uchakachuaji wa mafuta ya dizeli na petroli nchini ulikuwa asilimia 80 na hivyo kuwa chanzo cha uharibifu wa magari, mitambo inayotumia mafuta, mazingira na afya.

Mbali ya hayo, anasema, vitendo vya kuingiza mafuta kwenye soko ambayo hayajalipiwa kodi pia vilikithiri. Mafuta hayo ni yale ya kwenda nchi jirani, yaliyosamehewa kodi na ya magendo kutoka nchi jirani hasa kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini.

Kaguo anasema, hali hiyo ilisababisha kuwepo kwa ushindani usio sawa kwa wauzaji wa mafuta nchini na kuikosesha Serikali mapato. Kwa mfano, ilifikia hatua bei za mafuta Morogoro, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa zilikuwa rahisi kuliko Dar es Salaam.

Kaguo anasema, kufuatia udanganyifu huo, mwaka 2007, Ewura ilianza kuchukua sampuli za mafuta kutoka maghala ya mafuta na vituo vya mafuta ili kupima ubora kwa ajili ya kubaini uchakachuaji na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Hata hivyo, anasema, pamoja na hatua zilizochukuliwa, bado hazikuweza kumaliza tatizo la uchakachuaji kwani wapo wafanyabiashara wasio waaminifu ambao waliweza kuchakachua mafuta na bado yakakidhi viwango vya Shirika la Viwango (TBS).

Vile vile, Kaguo anasema, hata upimaji wa ubora kwenye maabara haukuweza kung’amua tatizo kwani mafuta hayo yalikuwa na sifa sawa na mafuta yenye ubora halisi.

Kufuatia hali hiyo, anasema, Ewura iliona suluhisho ilikuwa ni kutafuta teknolojia ambayo inaweza kung’amua uchakachuaji na uingizwaji wa mafuta ambayo hayajalipiwa kodi hata ukifanyika kwa kiwango kidogo, ndipo ikaonekana kuwa teknolojia sahihi ilikuwa ni kuweka vinasaba kwenye mafuta inayotumika na nchi mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Kaguo, katika kipindi cha kuanzia Januari 2001 hadi Desemba 2005, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitekeleza mradi wa kuweka vinasaba kwenye mafuta ambapo kampuni ya ukaguzi ya SGS ilipewa kazi hiyo. Anasema, hatua hiyo, ilileta mafaniko hasa katika kudhibiti uchakachuaji na uingizaji mafuta yasiyolipiwa kodi nchini. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali za kisheria na tekinolojia, TRA haikuweza kuendelea kutekeleza mradi huo.

Anasema, baada ya TRA kusitisha mradi wa kuweka vinasaba kwenye mafuta mwaka 2005, vitendo vya uchakachuaji wa mafuta na uingizaji mafuta yasiyolipiwa kodi nchini, vilikithiri.

Ni kwa kwa kuzingatia hali hiyo, Kaguo anasema, mwaka 2010 Ewura ilianzisha Programu ya Uwekaji Vinasaba kwenye mafuta ya petroli, dizeli, na mafuta ya taa yanayosambazwa nchini isipokuwa mafuta kwa ajili ya miradi maalumu ya maendeleo iliyosamehewa kodi na serikali.

Kwa mujibu wa Kaguo, hatua hii imewezesha kupunguza uchakachuaji wa mafuta nchini kutoka asilimia 80 hadi kufikia chini ya asilimia nne kwa sasa ambapo hali hii imedhihirika baada ya matumizi ya mafuta ya taa kupungua kutoka wastani wa lita milioni 30 kwa mwezi mwaka 2010 hadi kufikia wastani wa lita milioni tatu kwa sasa.

Anasema, teknolojia ya kuweka vinasaba imesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uingizaji mafuta ambayo hayalipiwi kodi na matumizi ya teknolojia hiyo yamechangia kuleta ushindani ulio sawa katika soko na mapato ya Serikali kuongezeka kufuatia ongezeko la kiasi cha mafuta kinacholipiwa kodi.

Hivyo, Kaguo anasema, kiasi cha mafuta ya dizeli kinachotumika nchini na kulipiwa kodi kimeongezeka kutoka wastani wa lita milioni 80 kwa mwezi mwaka 2010 hadi kufikia wastani wa lita milioni 184 kwa sasa. Vile vile, kiasi cha mafuta ya petroli kinachotumika nchini na kulipiwa kodi kimeongezeka kutoka wastani wa lita milioni 40 za mafuta kwa mwezi mwaka 2010 hadi kufikia wastani wa lita milioni 136 kwa sasa.

TEKNOLOJIA YA VINASABA NI NINI

Kaguo anasema, teknolojia ya vinasaba inahusisha kuweka kemikali maalumu kwenye mafuta ambayo inaweza kutofautisha nishati husika na mafuta ambayo hayajawekewa kemikali husika.

Pia, anasema, teknolojia hii inatakiwa kuwa na vifaa maalumu vya kupima na kung’amua kwa usahihi mkubwa mafuta yenye kiwango stahiki cha vinasaba na yale ambayo hayana au yana kiwango pungufu.

UMUHIMU WA VINASABA

Kwa mujibu wa Kaguo, umuhimu wa kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kuweka vinasaba kwenye mafuta nchini ni mkubwa kuendelea kudhibiti tatizo la uchakachuaji na kulinda ubora wa mafuta.

Hata hivyo, Kaguo anasema, pamoja na serikali na Ewura kuchukua hatua hizo, bado ipo mianya ambayo inaweza kutumika na wafanyabiashara wasio waaminifu kufanya uchakachuaji wa mafuta.

Kwa mfano, anasema, upo uwezekano wa mafuta ya taa ya magendo kutoka nchi jirani kutumika kwa uchakajuaji hasa mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwani tofauti ya kodi za mafuta ya taa na mafuta ya dizeli ni Sh 53 na mafuta ya petroli ni Sh 177.

Anasema, tofauti hizi ni kivutio cha uchakachuaji kwa wafanyabiashara wenye tamaa hususani bei ya mafuta ya taa inapokuwa chini katika soko la dunia ikilinganishwa na bei ya mafuta ya dizeli na petroli.

Anasema, kuna aina mbalimbali za vichakachuzi yakiwemo mafuta yanayobaki baada ya kusafishwa gesi asilia (condensate) na mafuta ya ndege (Jet–A1) yanayoweza kutumika kuchakachua mafuta. Kiasi cha condensate kinachozalishwa nchini kwa mwaka ni lita milioni 6.7.

Kaguo anasema,udhibiti huo umeokoa gharama za matengenezo ya magari na mitambo, kuokoa pesa za kigeni zinazotumika kuagiza mitambo na vipuri vinavyoharibiwa na uchakachuaji wa mafuta.

Anasema, tatizo la kuingiza kwenye soko mafuta ambayo hayalipiwi kodi litaendelea kudhibitiwa na hivyo kulinda ushindani kwenye soko na ukwepaji wa kodi. Anasema, bado ipo mianya ambayo inaweza kutumika na wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza kwenye soko mafuta kutoka nje ya nchi ambayo hayalipiwi kodi kodi.

Mfano anasema, pamoja na kuwepo kwa njia nyingine za kudhibiti mwenendo wa mafuta yanayosafirishwa nje ya nchi zinazotumiwa na TRA ikiwemo kuweka lakiri na eletronic tracking system, upo uwezekano wa wafanyabiashara kufanya hujuma na kuingiza mafuta yanayosafirishwa nje ya nchi kwenye soko la ndani ya nchi.

Hivyo, Kaguo anasema, teknolojia ya vinasaba inaweza kung’amua mafuta ambayo hayajawekewa vinasaba na kurahisisha kuwanasa wafanyabiashara wanaouza nchini, mafuta yanayosafirishwa nje.

Anasema, wastani wa mafuta yanayoagizwa kwa ajili ya kwenda nchi jirani ni lita bilioni 2.4 kwa mwaka. Kwa mfano, asilimia tano ya mafuta yanayokwenda nje ikiingizwa kwenye soko ni sawa na lita milioni 120 na Serikali itakosa zaidi ya Sh bilioni 80 na kuharibu ushindani.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 ulionesha kwamba kulikuwa na ongezeko la kodi la Shilingi bilioni 468.5 lililotokana na utekelezaji wa mradi wa uwekaji vinasaba kwenye mafuta nchini.

Hivyo, Kaguo anasema, kwa kuzingatia takwimu hizi, kuendelea kuweka vinasaba kwenye mafuta kunaokoa Shilingi bilioni 156 kwa mwaka. Aidha, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mafuta kwa sasa, ni dhahiri mradi wa uwekaji vinasaba unaokoa Shilingi bilioni 270 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 156 mwaka 2013.

Hata hivyo, Kaguo anasema, upo uwezekano wa wafanyabiashara kuingiza nchini mafuta ya magendo hususan maeneo ya mipakani ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini ambapo yakiweza kuingizwa kwenye soko, Serikali itaendelea kukosa mapato na kuharibu ushindani.

CHANGAMOTO ZA KUWEKA VINASABA

Kwa mujibu wa Kaguo, mradi wa uwekaji vinasaba una gharama ambapo ni mzigo wa walaji wa mafuta. Kwa sasa, gharama ambazo analipa mwananchi ni Shilingi 14 kwa lita, lakini unaokoa kodi ya zaidi ya Shilingi 800 kwa lita moja.

Anasema, pamoja na kuwa gharama za utekelezaji wa mradi wa kuweka vinasaba ni shilingi bilioni 40 kwa mwaka, Serikali bado inaokoa zaidi ya shilingi bilioni 270 kwa mwaka.

Aidha, manufaa mengine ni kuwa na mtu huwa na uhakika wa mafuta ya kutosha na yenye ubora; soko lenye ushindani ulio sawa; na kuchochea uwezekezaji kwenye sekta ndogo ya mafuta.

Chanzo: www.habarileo.co.tz