Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwekaji vigingi hifadhi ya Serengeti wakamilika

Serengeti Vigingi.jpeg Uwekaji vigingi hifadhi ya Serengeti wakamilika

Mon, 1 May 2023 Chanzo: Mwananchi

Hatimaye kazi ya uwekaji wa vigingi kati ya vijiji sita na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa Wilaya ya Tarime imekamilika huku hifadhi hiyo ikiahidi kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo uchimbaji mabwawa katika vijiji hivyo.

Uwekaji vigingi ulianza rasmi Machi 27 mwaka huu ambapo hadi kukamilika vigingi 184 vimewekwa kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 31.03. Akizungumza wakati wa kukabidhi vigingi hivyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara leo Jumapili Aprili 30, 2023, Mhifadhi Mkuu wa Serengeti, Izunde Msindai amesema hifadhi hiyo imetenga zaidi ya Sh760 milioni kwaajili ya kuchimba mabwawa mawili.

“Tumejipanga kujenga mabwawa mawili mwakani pamoja na kukarabati mengine mawili yaliyopo lakini pia tumekwisha watambua vijana zaidi ya 400 kutoka katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ili wafanye shughuli ndogo ndogo za hifadhini waweze kujipatia kipato na hii inaanza mara moja,” amesema Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuleta mahusiano mazuri kati ya wananchi wa vijiji hivyo na hifadhi ya Serengeti. Akitoa taarifa ya uwekaji vigingi, mpima ardhi kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Sowa amesema kazi hiyo ilikumbwa na changamito kadhaa lakini imefanyika kwa ufanisi mkubwa. “Kulikuwa na uelewa mdogo kwa wananchi lakini mwisho wa siku walituelewa na wakawa wanatoa ushirikiano hadi leo tumehitimisha kazi yetu kwa mafanikio,”amesema Ameongeza kuwa ili vigingi hivyo viweze kudumu ni lazima kuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya wananchi na hifadhi hivyo kupendekeza kutekelezwa miradi ya maendeleo ya jamii katika vijiji vilivyo jirani na hifadhi. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Selemani Mzee amesema kukamilika kwa uwekaji huo wa vigingi ni mwanzo wa kufanyika kwa shughuli za maendeleo katika maeneo hayo hatua ambayo itawanufaisha wakazi wa vijiji hivyo na mkoa kwa ujumla. “Huu mgogoro umedumu kwa muda mrefu sana na kama mnavyojua penye migogoro hakuna maendeleo kwahiyo kwa hatua hii ya leo ni kwamba tunaanza moja safari ya maendeleo,” amesema Amewataka wakazi wa vijiji hivyo kuhakikisha kuwa wanakuwa walinzi wa vigingi hivyo na kufanya shughuli zao kwa kuzingatia mpaka wao na hifadhi kwakuwa hivi sasa mpaka unafahamika tofauti na zamani ambapo mpaka ulikuwa haujulikani kutokana na vigingi vya awali kuong'olewa. Vijiji vilivyohusika katika uwekaji wa vigingi ni pamoja na Nyandage, Gibaso, Kenyamosabi, Karakatonga, Kegonga na Masanga.

Chanzo: Mwananchi