Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwanja wa ndege, magari ya kutumia waya kuongeza watalii Ngorongoro

11190 Utalii+pic TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imepokea ujumbe wa wawekezaji zaidi ya 50 ili kuona maeneo ya kuwekeza katika eneo hilo ambapo utajengwa uwanja wa ndege eneo la Olduvai Gorge na kuanzishwa aina mpya ya utalii wa magari yanayotembea juu ya waya.

Mipango hiyo inatarajia kuongeza idadi ya watalii na mapato ya NCAA ambayo mwaka wa fedha 2017/18 yamevuka lengo baada ya kukusanywa Sh124 bilioni na lengo lilikuwa Sh121 bilioni.

Akizungumza kwenye ziara ya wawekezaji hao, Naibu Mhifadhi wa NCAA, Asangye Bangu alisema, ujenzi wa uwanja huo na kuanzishwa vivutio vipya vya utalii katika maeneo yaliyotengwa itakuwa fursa nyingine ya kuongeza watalii.

Alisema NCAA inahitaji wawekezaji wa ujenzi wa mahoteli, kambi za utalii, kuendesha utalii wa farasi, utalii na balloon na baiskeli.

Akizungumzia wawekezaji hao, Bangu alisema kwa muda mrefu wawekezaji wamekuwa wakiona maeneo lakini kumekuwa hakuna utaratibu wa kuyatangaza ili wakawekeze kwa lengo la kuongeza idadi ya wageni na muda wa kukaa.

“Kuna uwekezano mgeni kukaa mpaka siku saba hapa NCAA tofauti na sasa siku moja au mbili. Tumeona ni vyema tuweke mkakati mpya unaolenga kuongeza mapato kutoka kwenye utalii na tutakutana tena Julai 16, mwaka huu kwenye Jukwaa la wawekezaji eneo la NCAA," alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii nchini (Tato), Wilbard Chambulo aliomba kuwapo kwa uwazi katika maeneo ya uwekezaji ili kila mtu aweze kushiriki kushindana.

“Tunataka kuwe na uwazi awe Mtanzania au raia kutoka nje wote tukae mezani tushindane, mchezo wa kufichaficha uishe tunataka kushirikishwa kuijenga nchi yetu tunaweza na tunafaa,” alisema Chambulo.

Naye mkurugenzi wa kampuni ya Miracle Experience, Hasnai Sajan alionyesha kuvutiwa na kuwekeza kwenye magari ya kuvutwa hewani na waya pamoja na balloon eneo la Ngorongoro.

“Ushirikishwaji huu ni mzuri, tukipata fursa ya kuwekeza tunaweza kuongeza zaidi wageni, maeneo ya Ndutu, Bonde la Ngorongoro na Embakai yanafaa kuweka magari ya waya yanayopita hewani,” alisema Sajan.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa Tato, Henry Kimambo alisema uamuzi wa kuwashirikisha kwenye maandalizi ya GMP ni jambo muhimu kwani wao ndio wanaotumia bidhaa zitokanazo na uhifadhi.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ilianzishwa mwaka 1959 na ina ukubwa wa kilometa za mraba 8300.

Chanzo: mwananchi.co.tz