Serikali imesema itaendelea kujenga na kupanua miundombinu ya viwanja vya ndege ili kujihakikishia utoaji wa huduma ndani ya nchi na nchi jirani.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kukagua upanuzi wa njia ya kuruka na kutua ndege kwenye Uwanja wa Ndege Kigoma.
Kihenzile amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan inachukulia sekta ya uchukuzi kwa njia ya anga kama mishipa ya ukuzaji uchumi na shughuli mbalimbali za utoaji huduma kwa wananchi ndani na nje ya nchi, ndiyo maana imewekeza fedha nyingi kwenye maboresho, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege kwa ujumla.
Ameongeza kuwa kwa mantiki hiyo serikali inajenga miundombinu ya viwanja vya ndege nchini ili kulifanya taifa la Tanzania kuwa kubwa na lenye nguvu ya ushawishi kiuchumi kikanda na Kimataifa.