Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uuzaji korosho Tandahimba kizungumkuti

KOROSHO 2 Uuzaji korosho Tandahimba kizungumkuti

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha zaidi ya tani 183,000 za korosho zenye thamani Sh405 bilioni kuuzwa, baadhi ya wakulima mkoani Mtwara, bado wana korosho ghafi majumbani, wakidaiwa kusubiri kuziuzia kwa taasisi inayoitwa Uwakota, huku Bodi ya Korosho (CBT) ikikana kutoa kibali.

Inadaiwa kuwa taasisi hiyo iliwaonya wakulima hao kutouza korosho zao mnadani ambako kuna kuna bei ya chini na badala yake Uwakota ingezinunua kwa bei kubwa, hali iliyofanya wakulima wengi kubaki na korosho majumbani huku wakisubiri taasisi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Novemba 23, Diwani wa Viti Maalum Tandahimba, Amina Mpota amesema kuwa kikundi hicho kimekuwa kikitembea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo ikiwemo Kata ya Dinduma, kuwashawishi wakulima kutouza korosho zao mnadani.

“Yaani hawa Uwakota wamewaaminisha wakulima kuwa watanunua korosho kwa bei kubwa na kuwataka wasiuze korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo wakulima wameziweka majumbani wanawasubiria,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Tandahimba, Baisa Abdallah Baisa ambaye amezungunmza na mwandishi wetu, amesema kuwa Uwakota ni ni chama ambacho kinatoka na umoja wa wakulima wa korosho Tanzania.

“Nikiri kweli wakulima wanazo korosho majumbani wao, wanauza pale wakiona bei imewaridhisha...kubaki na korosho nyumbani kunapoteza mapato kwa halmashauri, hatuwezi kulazimisha wauze, rahisi sisi kupata mapato kwa korosho ghafi lakini ikibanguliwa huwezi kupata mapato kabisa,” amesema Baisa.

Nae Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushiriki cha Tanecu, Mohamed Mwinguku amesema kuwa wakulima wanapaswa kuwa makini na kuepuka kurubuni na Uwakota.

“Unajua hao wanayumbisha wakulima ambapo wanakaa kwa muda mrefu na korosho bila kuuza matokeo yake wanauza kwa bei ndogo, wasiwasikilize wauze korosho kwenye mfumo uliowekwa na Serikali,” amesema Mwinguku.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred amesema Novemba 8, 2023 Uwakota walipeleka barua ofisini kwake wakiomba kukusanya korosho kutoka kwa wanachama wao kwa lengo la kuziuza zikiwa ghafi na zilizobanguliwa.

Kwa mujibu wa Alfred, CBT iliyakataa maombi hayo kwa msingi kwamba haikuwa tayari kutoa kibali kingine kwa chama hicho, hivyo kuwataka wakulima kuuza korosho zao kupitia mfumo wa stakabadhi gharani ama soko la awali kupitia vyama vya ushirika.

“Bodi imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wa korosho wakishutumu viongozi wa Uwakota kutowalipa fedha zao, na jambo hili limeleta changamoto kubwa ambayo kimsingi inaondoa lengo halisi la umoja huo,” amesema na kuongeza;

“Hatujawapa kibali ikumbukwe kwamba katika msimu wa 2021/2022 CBT iliwapatia kibali cha kukusanya korosho kutoka kwa wakulima wao kwa lengo la kubangua na kuziongezea thamani matokeo yake baada ya kuuza na kupata pesa hizo baadhi ya wakulima hawakulipwa fedha mpaka leo.”

Mwananchi ilifanya jitihada za kuwatafuta viongozi wa taasisi hiyo kwa njia ya simu ambapo ilifanikiwa kumpata Said Mzee Mwaya aliyejitambulisha kama kiongozi wao akiwa safarini Dodoma.

Mwaya alikiri kutopata kibali msimu huu, jambo ambalo limemfanya aende Dodoma kuomba kuonana na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ili kufikisha malalamiko yake dhidi ya bodi hiyo.

Amesema kuwa ni kweli Bodi ya korosho imewanyima kibali na kutoa sababu kuwa kuna baadhi ya wakulima wanawadai pesa za misimu wa mwaka 2021/2022.

Mwaya amesema kuwa tuhuma hizo zimeelekezwa kwao licha ya kuweka wazi juu ya jambo hilo huku taarifa zikifikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Ni kweli korosho zetu tunazo majumbani zaidi ya tani 38 sisi tuko wanachama 1371 lakini wenzetu 16 ndio walitugeuka na kufanya bishara bila idhini ya taasisi yetu ndio maana tumeamua kupeleka malamamko yetu Takukuru,” amesema na kuongeza;

“Sisi tunataka kuuza korosho zetu wenyewe tulitafuta soko tayari na tuliona kuna kitu tutakosa sisi tulishatafuta soko letu wenyewe, tulikopa pembejeo kwenye mabenki tunadaidiwa zaidi ya Sh105 milioni lakini bado hatujalipa tulitegemea kuuza korosho ili kulipa na vibali vya kuuza tumekosa.”

Kiongozi huyo wa Uwakota alitumia nafasi ya kuongea na mwandishi wetu na kusema: “Kupitia gazeti hili tunaomba hii habari iweze kutoa msukumo kwa mamlaka zinazotukandamiza ziweze kuacha na kutupa fursa ya kukusanya mazao yetu na kuyauza wenyewe.”

Kwa mujibu wa Mwaya, wamefanya vikao mbalimbali ambapo waliwaondoa waliokuwa viongozi wao kupitia mkutano mkuu na kwamba licha ya kuwa na uongozi imara, bado wanaoneka kana kwamba ni sehemu ya viongozi waliopita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live