Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uunganishaji wa gesi asilia majumbani washika kasi

20eb48919dde8bf15a2de86928eef6cc Uunganishaji wa gesi asilia majumbani washika kasi

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MATUMIZI ya gesi asilia yameshika kasi baada ya kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya matumizi ya gesi majumbani itakayounganisha wateja 850 huku mabasi yaendayo haraka yakitarajiwa kutumia nishati hiyo hatua ambayo imeelezwa kuwa itawezesha nauli kushuka.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema katika mwaka huu wa fedha limejipanga kuingiza gesi kwa wateja 1,000 huku kukiwa na mfumo utakaowezesha kuinunua kwa njia ya simu au benki.

Uzinduzi wa awamu hiyo ya pili wa matumizi ya gesi asilia kwa wateja wa majumbani ulifanyika jana katika mtaa wa Nzasa –Sinza katika wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa TPDC,James Mataragio alisema katika mwaka huu wa fedha Shirika limetenga Sh bilioni 10 kwa ajili ya kuunganisha wateja wa majumbani wapatao 1,000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

Alisema mradi uliozinduliwa jana utaunganisha wateja 506 ambao kati yao, 170 ni kutoka maeneo ya Sinza na wateja 336 ni wa Police Barracks-Mgulani.

Mitambo ya kupunguza mgandamizo wa gesi (PRS) iliyofungwa Police Barracks itakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja hadi 850. Dk Mataragio alisema mkandarasi wa mradi huo utakaogharimu Sh.

Bilioni mbili ni kampuni ya Tanzania ya BQ Contractors Limited iliyopatikana baada ya kutangazwa zabuni ya kimataifa na utakamilika katika miezi 12 .

“Mteja atalipia gesi asilia kadiri anavyotumia ,TPDC kwa kushirikiania na taasisi za eGA inaendelea kukamilisha mfumo, utamuwezesha mteja wa gesi ya kupikia majumbani kuwa na uwezo wa kununua gesi kwa njia ya simu au benki” alisema

Inakadiriwa kuwa matumizi ya gesi asilia kwa familia ya watu sita ni Sh 29,000 kwa mwezi sawa na wastani wa Sh. 1,000 kwa siku kwa matumizi ya kupikia vyakula vya aina zote kutokana na makadirio kutoka takwimu za wateja waliotumia gesi hiyo kwa muda mrefu.

Akizindua mradi huo, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani alisema matumizi ya gesi asilia yanazidi kuongezeka kwa kuwa na viwanda 48 na magari zaidi ya 800 yanayotumia gesi asilia.

Alitaka ujenzi wa mradi huo wa Nzasa kukamilika ndani ya miezi sita na siyo 12 kama walivyotaka. Aliwataka vijana wa mitaa ya hapo kuchimba mashimo na kazi nyingine kufikia Juni wananchi waanze kutumia gesi katika mitaa hiyo.

Alitaka TPDC kuhakikisha wanaingiza gesi kwa wananchi wote bila kujali kama miundombinu imepangwa au la kwani wananchi hao wameishajenga na nyumba haziwezi kubomolewa hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu.

Waziri Kalemani alipiga marufuku kutumia mabomba au luku za gesi kutoka nje ya nchi kwani tayari kuna viwanda viatu vinavyozalisha mabomba na luku. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Ronald Rwakatare alisema matumizi ya gesi asilia kwenye mabasi hayo yatapunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 45 kulingana na hesabu ya wataalamu wa TPDC.

Alisema uwapo wa gesi utasaidia kupata nafuu ya nauli anayolipa abiria na kwamba katika awamu ya kwanza inayohusisha njia katika Barabara ya Morogoro kwenda Kivukoni, Morocco na Gerezani, wanabeba abiria 200,000 hadi 500,000.

Mhandisi Dora Ernest kutoka TPDC alisema tayari michoro ya kihandisi imekamilika katika ujezi wa kituo cha DART Ubungo ikiwamo kufanyika kwa usanifu wa kina.

Chanzo: habarileo.co.tz