Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utoaji mikopo ya halmashauri wasitishwa kwa siku 30

Pic Fedha Data Wastaafu Marufuku hiyo inakuja ili kupisha uchunguzi

Wed, 27 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali mkoani Mwanza imesitisha utoaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ndani ya siku 30 ili kupisha uchunguzi baada ya kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa utolewaji wa fedha hizo kinyume cha kanuni na sheria za mikopo hiyo.

Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Robert Gabriel katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jana Aprili 25, 2022 ilibainisha kuwepo kwa mapungufu 12 yaliyokiukwa wakati wa utolewaji wa fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019 hadi 2021) na kusababisha upotevu wa fedha nyingi za Serikali.

“Tumesitisha utoaji wa fedha hizo ndani ya siku 30 ili kupisha uchunguzi kwa kamati zinazohusika na utoaji wa mikopo lakini pia kufanya ufuatiliaji wa kina wa fedha zilizotolewa ili wale waliochukua kinyume na taratibu wazirudishe,” amesema Gabriel.

Mhandisi Gabriel akibainisha mapungufu hayo, amesema kufuatia tume aliyoiunda kuchunguza utolewaji wa mikopo hiyo ilibaini wapo watumishi wa umma na wenye ajira walibainika kuchukua fedha hizo kinyume cha sheria na kanuni za utoaji wa mikopo na pia ilibaini kuwepo kwa vikundi hewa zaidi ya 34.

Tume hiyo pia ilibaini uidhinishwaji wa fedha bila nyaraka za mwenyekiti wa serikali ya mtaa na mtendaji wa eneo husika, vikundi kukosa uthibitishwaji, vikundi kushindwa kurejesha fedha kwa kipindi husika na kamati ya utoaji wa mikopo kushindwa kutoa matangazo.

Mapungufu mengine ni uwepo wa vikundi ambavyo vilichukua fedha bila kukamilisha mikopo ya awali, vingine vilichukua fedha bila kutia saini, vikundi vingine vilipata mikopo hiyo bila maombi ya mikopo kupitia kwenye vikao.

“Tunatoa rai kwa watumishi wa umma waliochukua fedha hizo kuzirudisha mara moja ili vikudi vingine vinavyokidhi matakwa viweze kuchukua fedha hizo.

“Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ipo kazini kuchunguza. Pia Jeshi la Polisi nao wapo kazini kufuatilia mienendo yote ya utolewaji wa fedha hizo ili wale waliokiuka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema Mhandisi Gabriel.

Amesema fedha hizo ni za serikali na haziwezi kupotea, hataonewa mtu na mkoa hawatakubali kuona fedha ya serikali ikichezewa.

“Lengo ni kurudisha nidhamu ya usimamizi wa mali ya umma na zaidi kuwa na huruma kwa vijana ambao wana kiu ya kubadilisha maisha yao kupitia fedha hizo,” amesisitiza.

Amewataka wale waliochukua fedha hizo na kwenda kuzigawa wajiorodheshe na kuzirudisha mapema na kwa utaratibu.

​Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Mkoa wa Mwanza ulitoa zaidi ya Sh8.778 bilioni kwenye vikundi vya wajasiriamali wadogo na hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu nusu ya fedha hiyo ilikuwa haijarejeshwa.

Mwaka jana, Nukta Habari, alitoa ripoti maalum inayoonyesha mwenendo usirodhisha wa utoaji mikopo hiyo katika mkoa huo ambapo kulikuwa na malalamiko kuwa inatolewa kwa upendeleo na itikadi za vyama huku baadhi ya watumishi wakidai rushwa kuwapatia wahusika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live