Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utekelezaji mkakati wa kukabili umasikini Njombe waiva

Bashe Pic Parachichi Utekelezaji mkakati wa kukabili umasikini Njombe waiva

Fri, 10 Feb 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mkoa mchanga zaidi nchini ulioanzishwa Machi mosi 2012 ukimegwa kutoka Mkoa wa Iringa, unazo wilaya nne ambazo ni Njombe, Wanging’ombe, Makete na Ludewa zenye halmashauri sita.

Mkoa huu wenye eneo la kilomita 24,994 za mraba zikiwamo kilomita 21,172 za ardhi zinazofaa kwa kilimo ambazo mkuu huyo wa mkoa anaamini ni kila kitu kinachohitajika kuwaondoa kwenye umasikini wakazi wake 889,946 waliohesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mtaka aliyeteuliwa kuuongoza mkoa huo Julai mwaka jana akitoka kuwa mkuu wa Mkoa wa Dodoma, anaamini iwapo juhudi zaidi zitaelekezwa kwenye kilimo ambacho wakulima wengi wanajihusisha na maparachichi, chai, ngano, mahindi, viazi mviringo na mazao ya misitu, kipato cha wananchi kitaimarika.

Maparachichi ni dhahabu ya kijani kwa wananchi wengi kwa siku za hivi karibuni kwani wengi wanayategemea kuinua kipato binafsi hata cha kaya.

“Imefika hatua kila kaya ina mti wa maparachichi, hii ni dhahabu ya Njombe,” anasema Ernest Ndendya, mkulima wa mkoani Njombe.

Mtaka anasema hakuna asiyejua faida za matunda hayo mkoani Njombe kwani ni zao lililoingizwa kwenye mkakati wa kuondoa umaskini wa kaya.

Mtaka ametoa msimamo huo kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) akisisitiza kuwa kukiwa na nia ya dhati, kila kitu kinawezekana.

Utekelezaji wa mkakati

Matamanio ya Mtaka kuubadili uchumi wa Njombe hayajaja ghafla kwani muda mfupi tangu alipoapishwa kushika majukumu yake alisema ndani ya miaka mitatu, kama ataendelea kuwepo, anatamani kusiwe na familia masikini inayonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Kusaidia Kaya Masikini Tanzania (Tasaf).

Alisema hilo linawezekana kwani Njombe ina utajiri wa hali nzuri ya hewa, udongo wenye rutuba, wananchi wenye utayari wa kufanya kazi kwa bidi na viongozi walio tayari kushirikiana nao kuimarisha kilimo cha mbogaboga, matunda, miti, ngano, vanila, shayiri, viazi mviringo, chai, matufaa (apple) na ufugaji ng’ombe pamoja na kuzitumia fursa za uvuvi na utalii zilizomo Ziwa Nyasa.

Katika kuhakikisha kaya zinazohudumiwa na Tasaf zinaondoka huko, tayari zimeanza kupewa miche 10 ya maparachichi kama mtaji wa kuanzia kuwaondoa wahusika kwenye lindi la umasikini.

Matarajio ya Serikali kwenye mkoa huo, Mtaka “hatuwezi kuwa viongozi kama hatuna ajenda. Ajenda yetu kubwa ni kuinua uchumi wa mkoa huu.”

Kati ya watu ilionao, ni 25,000 tu ndio wanapata ruzuku ya Tasaf. Mpaka sasa, takwimu zinaionyesha jumla ya kaya 1,885 katika Mji wa Makambako zimepewa miche 10 ya matunda hayo yenye soko la uhakika ndani na nje ya nchi ambazo baada ya miaka mitano ijayo zitakuwa na kipato cha uhakika hivyo kutotegemea tena ruzuku.

“Waziri wa Kilimo, (Hussein) Bashe ametupa miche 20,000 yenye thamani ya Sh100 milioni. Kaya zilizopewa miche hii zitaendelea kuwa chini ya Tasaf mpaka zitakapoanza kunufaika na maparachichi watakayoyavuna,” anasema Mtaka.

Mche mmoja wa mparachichi uliotunzwa vizuri, taarifa zinaonyesha unaweza kuzalisha Sh100,000 katika mwaka wake wa kwanza wa mavuno yaani miaka mitatu baada ya kupandwa na Sh150,000 kwa mwaka wa pili na Sh200,000 kuanzia mwaka wa tatu wa mavuno.

“Miche hii 10 itazalisha Sh2 milioni kwa mwaka wa kwanza na Sh6 milioni mwaka wa tatu wa mavuno, hawa wote watakuwa wameondoka kwenye umaskini,” anasema Mtaka.

Ili kuimarisha kilimo hasa cha matunda mkoani humo, Wiara ya Kilimo imeahidi kutoa miche 250,000 ya miparachichi kwa wanufauka wote 25,000 wa Tasaf mkoani Njombe.

Mbali na maparachichi, Mtaka anasema Wilaya ya Makete imetengwa iwe eneo maalum kwa ajili ya kuzalisha ngano ambazo Tanzania inaagiza kiasi kikubwa kila mwaka kutoka nje ya nchi hivyo kupoteza mabilioni ya shilingi.

Kumbukumbu zinaonyesha Tanzania inatumia tani milioni moja za ngano kila mwaka lakini uzalishaji wake wa ndani ni tani 600,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 400,000.

“Tayari tani 80 za mbegu ya ngano zimeletwa na wakulima watagawiwa hivi karibuni. Nimewasiliana na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ili wapime udongo kwa ajili ya kilimo hicho,” anasema Mtaka.

Anold Mhongole, mkazi wa Kibena anasema mkakati wa kukabiliana na umasikini mkoani humo utafanikiwa kutokana na juhudi kubwa kuelekezwa kwenye kilimo.

“Mie mwenyewe nilianza na miti mitano tu lakini sasa hivi ninayo 60 na navuna mamilioni ya fedha kwa maparachichi,” anasema Mhongole.

Ukusanyaji mapato safi

Ndani ya miaka mitatu ya kuendelea kuwa mkuu wa mkoa huo, Mtaka anatamani kuona kila kaya inakuwa na ng’ombe mmoja wa maziwa, familia zote kuwa na bima ya afya na kujenga mkoa utakaoongoza kwenye mitihani yote ya kitaifa kuanzia shule za msingi mpaka sekondari huku vyuo vya ufundi vikitoa hamasa uzalishaji wa kisasa pamoja na uwanja wa ndege kujengwa ili Hifadhi ya Taifa ya Kituro ifikike kwa urahisi.

Kati ya vitu vinavyo mwongezea Mtaka kuamini kwamba atatimiza ndoto alizonazo ni nguvukazi makini iliyopo kwenye halmashauri zote sita za mkoa huo.

Mpaka mwaka 2021, Mkoa wa Njombe ulikuwa na jumla ya wafanyakazi 4,559 wakiwamo waajiriwa 3,883. Idadi hiyo ilipanda kutoka wafanyakazi 4,443 waliokuwapo mwaka 2019.

Ripoti ya Mwenendo wa Uchumi wa Taifa ya mwaka 2022 inaonyesha mishahara ya wafanyakazi hao iliongezeka kutoka zaidi ya Sh6.98 bilioni mpaka Sh8.45 bilioni katika kipindi hicho.

Katika miaka hiyo mitatu, wafanyakazi hao kwa kushirikiana na wanachi wanaowahudumia waliongeza thamani ya uchumi wa mkoa huo kutoka Sh42.74 bilioni mwaka 2019 mpaka Sh51.71 bilioni mwaka 2021.

Katika mwaka wa fedha uliopita (2021/22), halmashauri tano zilivuka malengo ya makusanyo ya mapato. Halmashauri ya Wilaya ya Makete iliongoza baada ya kukusanya Sh3.88 bilioni sawana na asilimia 130 kutoka Sh2.98 bilioni zilizokisiwa.

Ya pili kwa ufanisi mkubwa ilikuwa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe iliyokusanya Sh3.96 bilioni sawa na asilimia115 kutoka Sh3.44 bilioni zilizokisiwa halafu Halmashauri ya Mji wa Njombe iliyokisia kukusanya Sh8.13 bilioni lakini ikapata Sh8.47 bilioni sawa na asilimia 104 kama ilivyokuwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa iliyopata Sh2.32 bilioni sawa na asilimia 104. Ludewa ilipanga kukusanya Sh2.23 bilioni.

Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe iliyopanga kukusanya Sh4.18 bilioni ilifikisha kiasi hicho hivyo kuwa na ufanisi wa asilimia 100. Ni Halmashauri ya Mji wa Makambako pekee ambayo haikufikia lengo baada ya kukusanya Sh3.07 bilioni sawa na asilimia 95 kutoka Sh3.22 bilioni ilizopanga.

Kwa CAG mambo safi

Hata ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inautaja Mkoa wa Njombe kusimamia vizuri mapato yake.

Kwenye ukaguzi alioufanya kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa, CAG anasema halmashauri nyingi hazikutenga asilimia 40 ya mapato yake na kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo kama sheria inavyotaka.

Hata hivyo, CAG anasema Halmashauri ya Mji wa Njombe iliongoza kwa kutumia asilimia 51 ya mapato yake ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma na halmashauri za Wilaya za Njombe na Mkuranga zilizotumia asilimia 46 ya mapato yasiyolindwa.

Wakati Mkoa wa Njombe ukiingiza halmashauri mbili kwenye orodha hiyo, CAG anasema Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ilikuwa ya mwisho kwa kutumia asilimia 16 tu ikifuatiwa halmashauri za Wilaya za Gairo na Bunda zilizotumia asilimia 17 ya mapato yasiyolindwa.

“Uchambuzi wa matumizi unaonesha kuwa zipo baadhi ya halmashauri ambazo zina uwezo mkubwa wa kuchangia zaidi ya kiwango cha chini kilichowekwa cha asilimia

40 au 60. Hivyo, katika mwaka wa fedha wa 2022/23 halmashauri tano zimewekwa kwenye kundi la kuchangia asilimia 70 kwa mwaka,” amesema CAG kwenye ripoti hiyo yam waka 2020/21.

Chanzo: mwanachidigital