Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata rubi ya Tanzania inayopigwa mnada Dubai

Utataapiic Utata rubi ya Tanzania inayopigwa mnada Dubai

Fri, 15 Apr 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Tanzania inatarajia kuvunja rekodi katika tasnia ya madini itakapolitambulisha jiwe la rubi nyekundu la kilo 2.8 katika maonyesho ya vito yaliyoandaliwa na Kampuni ya SJ Gold and Diamond.

Maonyesho hayo yanayojulikana kama Callisto Collection, yanafanyika leo huko Dubai.

Hata hivyo, Mwananchi ilipozungumza na Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko kuhusiana na suala hilo, alisema wizara yake haina taarifa lakini itafuatilia jambo hilo na Jumatano ijayo itatoa taarifa.

“Tunafuatilia jambo hili, hawa watu wangeeleza ukweli hii rubi imetoka wapi. Lakini hadi Jumatano next week (wiki ijayo) tutajua, maana hata aliyepeleka hatumjui,” alisema Dk Biteko.

Rubi hiyo inayodaiwa kuwa na thamani ya Sh276 bilioni (Dola 120 milioni za Marekani) ilichimbwa katika Kijiji cha Winza wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.

Inaelezwa kuwa Tanzania inakwenda kuweka historia ya kipekee katika maonyesho hayo yatakayoipa nafasi dunia kujionea rubi hiyo nyekundu.

Dubai itakuwa jiji pekee litakaloitambulisha duniani kwenye maonyesho hayo ya vito yaliyoandaliwa na Kampuni ya SJ Gold and Diamond, yakijulikana kama Callisto Collection.

“Uzinduzi wa maonyesho ya Callisto Collection hapa Dubai ni ya kihistoria kwa kampuni iliyoyaandaa kwa kuwa itajitambulisha duniani kuwa ni miongoni mwa zinazoongoza kwa uhifadhi wa madini ya vito, ikiwa na hazina ya Dola 4 bilioni za Marekani inayojumuisha dhahabu na vito vingine,” alisema Patrick Pilati, mkurugenzi mtendaji wa SJ Gold and Diamond.

Baada ya maonyesho hayo, rubi hiyo itakuwa wazi kwa mnada baada ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani. Rubi hiyo inatarajiwa kuuzwa si chini ya Dola 120 milioni za Marekani (Sh276 bilioni).

Machimbo ya Winza yanayopatikana katika ukanda wa Usagara, yaligunduliwa mwaka 2007 na ni maarufu kwa madini hayo ya vito.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz