Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata hisa asilimia 31.5 mgodi Mwadui kutaka kuuzwa

Kuzama Mgodini Utata hisa asilimia 31.5 mgodi Mwadui kutaka kuuzwa

Wed, 16 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Kampuni ya uchimbaji madini ya Caspian inakaribia kuwa mmiliki wa asilimia 31.5 ya hisa za mgodi wa almasi uliopo Mwadui mkoani Shinyanga ambao kwa sasa uko chini ya kampuni ya kimataifa ya Petra Diamond.

Katika uendeshaji wa mgodi huo, Serikali inamiliki asilimia 37 ya hisa, huku Petra ikimiliki asilimia 63, ambazo kampuni hiyo imeamua kuingia mkataba wa awali (MoU) wa kuuza nusu yake (asilimia 31.5) kwa Caspian, kama inavyojielezwa katika taarifa ya Petra iliyotolewa kwa umma mwaka jana.

Hata hivyo, Serikali imesema haina taarifa za kimaandishi hivyo haitakuwa tayari kuridhia makubaliano hayo, hadi itakaposhirikishwa na kujiridhisha kama mbia mwenza.

Shughuli za uzalishaji wa almasi katika mgodi huo ziko chini ya Kampuni tanzu ya Williamson Diamonds Limited (WDL), iliyoporomoka uzalishaji, kutokana na matengenezo kabla ya kuimarika mwaka jana.

Chanzo cha habari kinaeleza uwezekano wa Caspian inayomilikiwa na mfanyabiasra Rostam Aziz kununua hisa hizo, utajulikana baada ya kikao cha bodi ya wakurugenzi ya Petra Desemba 2, mwaka huu.

“Kwa sasa sio sahihi kusema ameshapata hisa hizo, itategemeana na kikao hicho,” kilieleza chanzo hicho.

Taarifa ya Petra ilieleza baada ya kukamilika hatua zote kabla ya Juni mwaka 2023, Petra na Caspian kila moja itakuwa na hisa asilimia 31.5 katika WDL, huku Serikali ikiendelea kuwa na asilimia 37 iliyobaki.

Kauli ya Tume ya Madini

Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini nchini (TMC), Venance Kasiki alipoulizwa alisema Serikali haina taarifa hizo kimaandishi.

“Tunasikia tu, tulitegemea Petra amuulize mbia mwenza (Serikali) kama ana uwezo au la, kabla ya kutafuta mbia mwingine.

“Wakati wa Covid-19 (Uviko-19) ilikuwa kama hivyo, walitaka kuuza pia mgodi huo, tukawauliza kwa nini hawakuuliza mbia? wakakataa hawauzi na wakaomba radhi, ikaisha.

“Hili pia ni hear say (tunasikia). Kama wakileta ofa tutawakubalia, lakini tujue kwanza kimaandishi,” alisema Kasiki.

Petra ilitangaza kuuza mgodi huo mwaka 2020, huku Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo kwa wakati huo akinukuliwa na gazeti dada la The Citizen akikana Serikali kupewa taarifa rasmi.

Katika taarifa yake, Petra inayomiliki pia migodi ya Finsch, Cullinan na Koffiefontein (yote ikiwa nchini Afrika Kusini), ilisema: “Makubaliano haya yanakwenda sambamba na malengo ya kampuni ya Petra katika kupunguza vihatarishi vya kiuwekezaji, huku ikiendelea kulinda maslahi yake katika umiliki wa hisa hizo za WDL.”

Kuhusu hatua za malipo ya kikodi juu ya makubaliano ya mauzo ya hisa hizo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alidai kutokuwa na taarifa zozote kuhusu hatua hizo.

“Sina taarifa za jambo hilo kwa sasa, pengine ungecheki na FCC (Tume ya Ushindani)”

Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio alisema tume hiyo bado haijapokea fomu inayohusisha makubaliano ya kuuziana hisa hizo.

“FCC ndio inathibitisha makubaliano hayo, lakini watalaamu wangu wanasema bado haijatufikia. Sasa wanaweza kuendelea mpaka watakapokubaliana ndipo waje kwetu.”

Akifafanua kuhusu uhalali wa makubaliano hayo bila ushirikishaji wa Serikali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Petra Diamond, Richard Duffy alisema kwa njia ya barua pepe;

“Kwa sasa Petra iko katika mchakato wa kukamilisha makubaliano na Caspian, kisha itatafuta idhini muhimu za Serikali na udhibiti.”

Awali katika tukio la kusaini makubaliano hayo mwaka jana, Duffy alisema: “Tunafurahi sana kushirikiana na Caspian wanaoleta uzoefu mkubwa. Hili litatusaidia kuboresha kwa manufaa ya wadau wote wa WDL. Mpango wetu mpya na Caspian, unaiweka Williamson kwenye msingi imara sana kwa siku zijazo.”

Mgodi huo kati ya mwaka 2009/2017 ulikuwa umewekeza Dola za Marekani milioni 137, huku ukizalisha zaidi ya tani za carat milioni nne.

Mapato yaliongezeka kutoka Dola milioni 41.9 mwaka 2012 hadi Dola milioni 78.9 mwaka 2017 huku ukiwa na uwezo wa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.

Chanzo: mwanachidigital