Dodoma. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema wanawekeza katika maeneo mapya ya utalii ikiwemo utalii wa meli utakaoingiza Taifa pato la zaidi ya Sh1 trilioni kwa mwaka.
Maeneo mengine walioanza mchakato wa kuwekeza ni utalii wa mikutano, fukwe na utamaduni.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi juzi Jumanne Juni 4, 2019, Dk Kigwangalla amesema kwa mwaka 2019 wamefanikiwa kupata meli za utalii zaidi ya 11 zilizoingia Tanzania.
Amesema utalii wa meli ni eneo litakalosaidia kupata watalii wengi kwa muda mfupi na kwa jitihada za muda mfupi.
“Inakadiriwa kama tukiwekeza Sh150 bilioni tutapata zaidi ya Sh 1trilioni kwenye pato la Taifa katika eneo hili,” amesema.
Amebainisha kuwa tayari wameandika andiko kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili kutenga eneo na wanatarajia kutangaza zabuni Juni 2019 kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo.
Pia Soma
- Zimbabwe, EU wazungumzia vikwazo
- Uhuru azuia chupa za plastiki Kenya
- Mbunge CCM aomba waombewe wapite bila kupingwa 2020
Mbunge huyo wa Nzega Vijijini amesema watalii watapata nafasi ya kushuka na kwenda katika vivutio vingine vya utalii kabla ya kurejea katika meli.
“Hii iko katika hatua nzuri. Pia tutajenga utalii wa mikutano, utalii wa fukwe na utamaduni. Eneo limeshapatikana Kigamboni (jijini Dar es Salaam),” amesema.
Waziri huyo amesema tayari mradi umeshaandikwa na wako katika hatua za mwisho za kuupitisha ndani ya Serikali ili waanze kutekeleza.