Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'Utalii umerejea, tahadhari corona lazima ichukuliwe'

101998 KIGWANGALAA+PIC 'Utalii umerejea, tahadhari corona lazima ichukuliwe'

Sat, 30 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, amesema utalii nchini lazima uendelee licha ya kuwapo kwa janga la corona ambalo ni tishio duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa video maalum za kutambulisha utalii wa Tanzania, Dk. Kigwangalla alisema janga la corona limeathiri kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii nchini na hivyo kuathiri uchumi wa nchi pia.

Hata hivyo, waziri huyo alisema kwa sasa dalili za kurejea kwa utalii katika hali yake ya kawaida zimeanza kuonekana baada ya watalii kuanza kuingia nchini.

“Sasa hivi soko la utalii duniani limeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na ugonjwa wa corona, lakini nchi mbalimbali zimeamua kuanza kufungua biashara ya utalii na biashara ya usafiri wa anga na usafiri wa majini na zingine zinazoendana na sekta ya utalii.

“Kwa msingi huo, kama tungeendelea kuweka masharti yaliyokuwapo, sekta hii isingeweza kufunguka kama vile katika mataifa mengine walioanza kufungua utalii kwenye nchi zao," alisema.

Akizindua video hizo maalum zilizopewa jina ‘Tanzania Unforgettable’ (Tanzania Haisahauliki) zikitengenezwa kwa lugha mbalimbali zikiwamo Kiingereza, Kiswahili, Kichina, Kiisraeli na Kifaransa, waziri huyo alisema lengo lake ni kuitangaza Tanzania kiutalii katika mataifa mbalimbali duniani.

“Video hizi kuna ya dakika tatu, dakika saba na dakika 10. Ninatoa rai kwa Watanzania wote, wadau mbalimbali wa utalii, washiriki kuisambaza video hii ili kuwavuta wote na kukonga nyoyo za watakaoitazama video hiyo ambayo inaelezea vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania," aliomba.

Alisema wizara hiyo imeweka mwongozo ambao unaelekeza hatua muhimu za kufanya, ili kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona na kuwataka watalii na wananchi wanaohudumia watalii hao, kufuata mwongozo huo kujilinda dhidi ya hatari ya maambukizo ya corona.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live