Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utalii sasa kutangazwa kidigitali

Utalii Kifo Wiki ya Utalii yaadhimishwa

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wadau wa Utalii wametakiwa kutumia ubunifu zaidi katika kutangaza vivutio vya utalii wa ndani ili kukuza sekta ya utalii na kuongezea pato la taifa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga alipotoa salamu za Wizara katika Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 lililofanyika leo Mei 11, 2022 jijini Dar es Salaam.

“Kuna mambo yanayojitokeza katika mazingira ya sasa kwenye sekta ya utalii ambayo ni muhimu sana kuhusisha ubunifu wa teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii,” amesema Balozi Kasiga.

Balozi Kasiga ameeleza kuwa haiwezekani kuendelea kutangaza utalii kwa njia tulizokuwa tunatumia zamani, ndiyo maana wabunifu wa teknolojia wametuonesha mchango wa teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii na sasa tunaona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amejadiliwa sana kutokana na kutangaza uzinduzi wa filamu ya ‘Royal Tour’ ambayo imeelezea kwa undani vivutio vya utalii nchini kwa teknolojia ya juu zaidi.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mindi amewasihi wabunifu kuendelea kutumia teknolojia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.

Kupitia kongamano hilo washiriki wamejadili namna ubunifu na teknolojia vinaweza kutumika kama njia mbadala ya kutangaza vivutio vya utalii na kuwavutia watanzania waweze kutembelea vivutio hivyo.

Aidha, kupitia Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022, teknolojia ya ‘Safari Wallet’ imezinduliwa na kijana wa Kitanzania ambapo inapatikana katika tovuti ya ‘Safari Wallet’ na inatumika kuwasaidia wadau wa utalii kuchagua sehemu za kutembelea kwa urahisi na haraka zaidi vivutio vya utalii nchini

Balozi Kasiga ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itajitahidi kuiwasilisha teknolojia ya ‘safari wallet’ katika nyanja za kimataifa ikiwemo ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mataifa mengine ili kuweza kutangaza zaidi vivutio vya utalii nchini.

Naye Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Job Runhaar amesema teknolojia ni nyenzo muhimu katika kutangaza sekta ya utalii nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live