Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utajiri uliopo kwenye Kilimo cha Parachichi

49676b8873961e5dfdd9bb7435414de5 Zao la Parachichi

Tue, 3 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewahimiza wananchi walime zao la parachichi kwa kuwa faida yake ni kubwa.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu janailieleza kuwa, Majaliwa alisema hayo alipotembelea shamba la parachichi na kiwanda cha kuchakata zao hilo katika kijiji cha Ilolo, wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

Shamba linamilikiwa na kampuni za Kuza Africa na Moravian Farming PVT.

“Kilimo cha parachichi kina manufaa makubwa sana, wananchi ongezeni ukubwa wa mashamba ya parachichi na serikali italisimamia kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi masoko,” alisema Majaliwa.

Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa, Majaliwa ameziagiza halmashauri zote zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche ya zao hilo na kuigawa kwa wakulima.

Alisema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu na kuwataka wananchi walime kwa wingi ili wajikwamue kiuchumi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amewapongeza wawekezaji hao kwa kuwa wamewezesha wakulima kutatua changamoto ya soko la uhakika la zao la parachichi.

Alisema ingawa kuna soko la parachichi katika kiwanda hicho, pia serikali itahakikisha soko la parachichi za Tanzania linapatikana Afrika Kusini.

Meneja Rasilimali Watu wa kampuni hizo, Noel Kabuje alisema wamewezesha wakulima kupata soko la zao hilo kwa kununua matunda ya parachichi.

“Mbali na kulima parachichi, sisi wenyewe pia tunanunua matunda ya parachichi kutoka kwa wakulima wadogo, tunayachakata na kufungasha matunda ya parachichi na kuyauza nje,” alisema Kabuje.

Alisema kwa sasa wanauza parachichi Ujerumani, Italia, Ufaransa, Mashariki ya Kati, Uingereza na Hong Kong.

Chanzo: www.habarileo.co.tz