Wizara ya Kilimo imeendelea kufanya utafiti katika maeneo ya Mtwara ili kupata mazao mengine zaidi ya korosho, ambayo mkulima ataweza kuzalisha ili kuondokana na utegemezi wa zao la korosho pekee.
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo (Chadema) aliyetaka kujua, kuna mkakati gani wa kufanya utafiti ili kubaini mazao yanayoweza kulimwa na kustawi Mkoa wa Mtwara kama mbadala wa zao la Korosho.
Alisema Wizara ya Kilimo kupitia Tari imeendelea kuhamasisha kilimo cha mazao ya muhogo, ufuta, karanga, alizeti, njugumawe, choroko, mbaazi, mtama na kunde ambayo tayari yamefanyiwa utafiti na kuonekana yanafaa kulimwa katika wilaya zote za Mkoa wa Mtwara.
Alisema Wizara imetoa elimu ya kilimo bora cha mazao hayo ikiwemo matumizi ya mbegu bora, udhibiti wa visumbufu (wadudu waharibifu na magonjwa), kupanda kwa wakati na matumizi sahihi ya mbolea kupitia mashamba ya mfano, radio za kijamii na televisheni.