Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utafiti wabaini biashara ya vipeto kudorora

Vipeto Kudororoa.png Utafiti wabaini biashara ya vipeto kudorora

Thu, 23 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na kukua kwa uchumi na ongezeko la masoko ya mtandao, ungetarajia kuona takwimu za usafirishaji wa vipeto zinaongezeka, lakini takwimu rasmi zinaonyesha kinyume chake.

Kuongezeka kwa ushindani usio rasmi wa usafirishaji vipeto umetajwa kuwa sababu ya kushuka biashara hiyo kwa mashirika na kampuni zinazofanya shughuli hiyo.

“Biashara nyingi sasa hivi nafanya mtandaoni, nikiposti mtu akipenda ananiandikia nampa namba ya malipo, akishalipa namtumia popote alipo hata mkoani. Wanaokuja dukani siku hizi ni wachache,” anasema Khadija Salumu, muuza nguo wa jijini Dar es Salaam.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa ndani ya miaka mitano vipeto na vifurushi vilivyosafirishwa na Shirika la Posta Tanzania na kampuni binafsi za kusafirisha mizigo (courier) vimeshuka kwa takribani asilimia 70.

Vipeto na vifurushi vinavyokwenda ndani na nje ya nchi vilishuka kutoka milioni 10.8 mwaka 2018 hadi milioni 3.309 mwaka 2022, inaeleza Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kupungua kwa mizigo hiyo kunatajwa na wadau kuwa kunachangiwa na ushindani uliowekwa na mabasi ya abiria na malori ya kusafirisha mizigo.

Ripoti hiyo ya robo ya tatu ya mwaka inayoishia Septemba 2023 inaonyesha kabla ya kufikia hapo ilipo, mwaka 2019 uliongoza kwa kurekodi kiwango kikubwa cha mizigo iliyosafirishwa kwa njia hizo ambacho kilifikia milioni 12.153.

Baada ya mwaka huo, 2020 ndio ulikuwa mwaka wa kwanza kushuhudia anguko la huduma hiyo kwa karibu mara mbili na zaidi hadi kufikia milioni 5.1.

Idadi hiyo iliendelea kupungua hadi kufikia milioni 3.1 mwaka 2021 kabla ya kupungua zaidi kufikia milioni 3 mwaka jana.

Kwa upande wa biashara hiyo kimataifa, kiwango nacho kilishuka kutoka vifurushi milioni 5.09 mwaka 2018 hadi kufikia 937,124 mwaka 2022.

Hiyo ilienda sambamba na idadi ha mizigo iliyopokewa kutoka nje ya nchi ilifikia 394,152 mwaka 2022 kutoka milioni 7.99 mwaka 2018.

Kwa kipindi cha robo mwaka kilichoishia Septemba, jumla ya vifurushi 651,928 vilisafirishwa kwa njia ya posta, huku 152,584 vikisafirishwa kwa njia ya courier na asilimia kubwa ya mizigo hiyo ikisafirishwa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mizigo iliyosafirishwa kupitia njia hizo mbili, 522,348 ilikwenda ndani ya nchi, 211,460 nchi za Afrika ya Mashariki na 70,709 ilikwenda nchi nyingine duniani.

Kwa upande wa mizigo iliyoingia kutoka nchi za nje, mataifa tofauti na ya Afrika Mashariki yaliongoza kutuma idadi kubwa ya vifurushi nchini.

Jumla ya mizigo 97,238 iliingia nchini kutoka nchi za nje ikilinganishwa na mizigo 9,909 iliyotoka nchi za Afrika ya Mashariki, ripoti inasema mingi kutoka nje ililetwa na Shirika la Posta.

Utafiti muhimu

Akizungumzia anguko la biashara ya vifurushi, Dk Balozi Morwa, ambaye ni mtaalamu wa uchumi anasema kuna haja ya kufanya tafiti zaidi ili kujua sababu za kushuka kwa biashara hiyo katika zama hizi.

Anasema takwimu hizo zikifanyiwa utafiti itafahamika wapi kunapaswa kuwekwa nguvu zaidi ili kuhakikisha mizigo inasafirishwa katika utaratibu maalumu.

“Pengine hali ya sasa inachangiwa na ushindani uliopo katika usafirishaji mizigo, unaofanywa na mabasi pamoja magari makubwa ya mizigo, ambapo watu wanaumia sasa badala ya kutumia Shirika la Posta na kampuni za usafirishaji mizigo (courier),” alisema Morwa.

Anasema uwepo wa mwanya huo umekuwa ukifanya watu kurudia njia za asili zilizokuwa zikitumika zamani kufikisha mizigo, huku akibainisha kuwa kuna kipindi usafirishaji vipeto kiholela ulipigwa marufuku na ilifikia hatua basi haliruhusiwi kusafirisha hata bahasha.

Kwa upande mwingine, mtaalamu mwingine wa uchumi, Profesa Jehovaness Aikaeli anasema majanga yanayoikumbuka dunia kama ugonjwa wa Uviko-19 na Vita ya Ukraine vinaweza kuwa moja ya sababu ya kushuka kwa usafirishaji wa mizigo kutoka nje.

Profesa Aikaeli anasema sababu hizo mbili zilichangia kutikisika kwa uchumi kwa baadhi ya nchi, jambo ambalo lilifanya kiwango cha watu kununua bidhaa kushuka.

“Uagizaji bidhaa zetu pia unategemea utumaji wa fedha za kigeni, sasa kunapokuwa na vitu kama hivi kunapunguza uwezo wa watu kuagiza kama mwanzo na badala yake watu wanachagua kuweka akiba,” anasema Profesa Aikaeli.

Pia alisema matumizi ya Posta katika kutuma na kupokea mizigo inaonekana kama habari ya zamani kwa sasa kutokana na kuwapo kwa njia mbadala ambazo watu wanaweza kuzitumia tofauti na awali.

“Mabasi ya abiria yamekuwa sehemu kubwa ya usafirishaji mizigo kwa sasa, mtu anatuma mzigo sehemu za karibu baada ya muda anapokea mzigo wake, hivyo mabadiliko yanayotokea yanabadili pia namna ya kuenenda,” anasema.

Kwa mujibu wa Profesa Aikaeli, umefika wakati wa kuangalia namna Shirika la Posta linavyoweza kujiimarisha katika usafirishaji wa mizigo kwa kufanya maboresho katika utoaji huduma.

Ikiwa mzigo utapita ndani ya shirika hilo ni vyema kuhakikisha unafika kwa mhusika kwa wakati na bila changamoto yoyote.

“Kama mzigo wako unatoka leo na una uhakika utafika leo, mtu atakuwa hana sababu ya kuangalia sehemu nyingine, hivyo kuongeza ufanisi ni muhimu,” anasema msomi huyo.

Hata hivyo, Profesa Haji Semboja, yeye anasema mageuzi zaidi yanaweza kufanyika ikiwa watu wanaosimamia maeneo hayo watakuwa wabunifu na watapatikana kwa njia ya ushindani.

“Pia ni vyema kuangalia sheria za ushindani katika biashara, wajipange kufuatana na mahitaji ya soko, matumizi ya rasilimali watu, mifumo ya uendeshaji kampuni ziendane na mifumo mingine ya kimataifa,” anasema Profesa Semboja, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).

Profesa huyo anasema ni vyema kujifunza wengine wanafanya nini na uwepo ubunifu na ujanja katika kutafsiri sera za dunia.

Anaongeza kuwa huduma ya usafirishaji mizigo kupitia kampuni (courier) ilifanywa kuwa wa ushindani kwa taasisi binafsi pia, jambo ambalo limefanya watu kutumia njia tofauti, ikiwemo mabasi ya abiria, pikipiki na malori kufikisha huduma.

Urahisi na kuwahi

Wakizungumzia suala hilo, baadhi ya wananchi walisema urahisi wa kufikia huduma na kuwahi kwa mzigo ndiyo sababu ya wao kuchagua sehemu gani watume vifurushi vyao.

"Wakati mwingine ni mazoea, miaka yote nimezoea kutuma mizigo kwenye basi au nasubiri mtu awe anasafiri nimpatie aende nao nyumbani kwa wazee," anasema Joseph Mbwilu.

Hata hivyo, anasema matumizi ya Posta kwake yamekuwa katika nyaraka muhimu ambazo anahitaji uhakika wa kuwa salama.

Leila Ally alisema uwepo wa njia tofauti za kusafirisha mizigo huenda ndiyo sababu ya kuwapo kwa ushindani ambao umeshindwa kutoa namba halisi za mizigo iliyosafirishwa.

"Mizigo inayosafirishwa iko mingi sana, ni vile wameshindwa kufikia njia zote zinazotumika kusafirisha mizigo na kufanya hesabu, waangalie namna ya kufanya wasafirishaji mizigo hawa wanakuwa rasmi ili waweze kuwajibika kwa kitakachotokea," alisema Ally.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live