Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utafiti mbegu za kahawa zitakazo stahimili ukame waanza

Kahawa Pc Utafiti mbegu za kahawa zitakazo stahimili ukame waanza

Sun, 19 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

New Content Item (1) Kasulu. Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) inafanya utafiti wa aina nne za mbegu za kahawa zitakazoweza kukabiliana na maeneo yenye ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza Novemba 18, 2023 wakati wa ugawaji miche bora ya zao hilo katika kata ya Msambara iliyopo Halmashauri ya Kasulu Mji, Mtafiti na Usambazaji Teknolojia na Mafunzo, Jeremiah Magesa amesema wanatarajia tafiti hizo zitakuwa tayari na kuzisambaza kwa wakulima wa maeneo husika kwa mwaka 2025.

Magesa amesema utafiti huo umetokana na changamoto wanazokutana nazo wakulima ikiwemo baadhi ya maeneo kukosa mvua ambapo awali maeneo hayo yalikuwa yakipata mvua vizuri na kwa wakati hivyo wao kama Taasisi walichukua hatua za kufanya utafiti.

Amesema utafiti wa mbegu hizo unaendelea na wanafanya majaribio katika maeneo mbalimbali yenye ukame hapa nchini , ikiwemo Mkoa wa Kigoma eneo la kata ya Msambara Halmashauri ya Kasulu Mji, Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo maeneo hayo yatawakilisha maeneo mengine yenye hali hiyo.

“TaCRI ilichukua hatua ya kuanzisha majaribio ya kutathmini aina nne za mbegu zinazovumilia ukame zitakazotolewa mwaka 2025 kwa wakulima na kazi kubwa zitakuwa ni kuzizalisha na kuzisambaza kwenye maeneo yenye ukame ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”amesema Magesa

Baadhi ya wakulima wa kata hiyo ambao wanalima zao la Kahawa kwa mara ya kwanza, wamesema wanaomba kupatiwa mafunzo kuhusiana na zao hilo ili waweze kulima kwa tija na ufanisi ili wapate faida.

Mkulima wa zao la Kahawa, Edson Mtwe amesema awali alikuwa akilima mahindi ila akashawishika kuanza kulima zao la Kahawa ambalo halina magonjwa mengi na halihitaji mbolea nyingi ikilinganishwa na mazao mengine.

“Mimi nimehamasika kulima kilimo biashara ambapo awali nilikuwa nikilima mazao ya chakula, ombi langu ni wataalamu wasichoke kututembelea mara kwa mara kwasababu hatuna uzoefu wa zao hili na ni mara ya kwanza kulimwa katika kata yetu,”amesema Anjela Philimon

Mratibu wa zao la Kahawa Halmashauri ya Kasulu Mji, John Eliakimu amesema jumla ya miche 45,473 imetolewa kwa wakulima 180 wa kata za Heru juu, Msambara, Mganza na Luhita kwenye halmashauri hiyo huku, uzalishaji wake ukitarajiwa kuwa tani 157.5 kwa kipindi cha mavuno.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live