Utafiti wa Sayansi ya Malikale nchini umekuwa ni Moja ya chanzo Cha Mapato Serikalini na kwa mtu mmoja mmoja kutokana na makundi ya watafiti kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni kuja nchini Kwa Utafiti kwenye maeneo yenye Urithi adhimu wa Kihistoria.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu kwenye Bonde la Olduvai ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mkoani Arusha, alipokuwa akikagua Shughuli za utafiti zinazofanywa na Wataalam wa ndani na wa Kimataifa wa Akiolojia.
Dkt. Ntandu amesema kuwa Tanzania inaendelea kupokea watafiti wa Akiolojia kutoka nchi mbalimbali kutafiti kwenye maeneo ya Malikale yaliyopo sehemu mbalimbali nchini hususani eneo la Olduvai lenye historia kubwa ya ugunduzi wa masalia ya Binadamu wa Kale wanaosadikika kuishi kuanzia Miaka Milioni 1.7 iliyopita.
Aidha Dkt. Ntandu ameongeza kuwa watafiti hao wanapoingia nchini wanahitaji kufanya Matumizi mbalimbali hususani malazi, chakula, Mawasiliano, Usafiri, kulipia ada ya utafiti, pamoja na kuwapatia ajira za muda mfupi wasaidizi wao jambo linaloingizia Taifa fedha za kigeni na kutoa ajira Kwa watanzania.
"Watafiti hawa ni wadau wetu muhimu sana, ukiachana na Matumizi yao mengine, matokeo ya tafiti zao husaidia kuvutia Watalii nchini, pamoja na watafiti wengine hivyo nchini kuendelea kupata mapato, ndio maana nilikuja kukutana nao ili kuona na kukagua tafiti zao na kupata uwelewa wa pamoja juu ya namna nzuri ya kuendeleza tatifi hizi” Dkt. Ntandu
Akizungumzia utafiti wao, Profesa Fernando Diez Martine kutoka Chuo Kikuu Valladolid nchini Hispania, amesema wameamua kuja Tanzania kufanya utafiti kwa kuwa ni nchi yenye Utajiri Mkubwa wa Urithi wa Malikale pamoja amani na Utalivu unaowafanya wafanye kazi zao za kitafiti kwa maana, huku akiipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuhifadhi vyema Maeneo ya Malikale kwa faida ya kizazi cha sasa na Kijacho.