Dar es Salaam. Wakati biashara za mtandaoni zikiendelea kushika kasi na kutoa ajira kwa vijana nchini, utafiti umebaini kuwa wengi wanaofanya kazi hizo hawana mikataba rasmi hivyo kukosa haki za msingi za ajira.
Hali hiyo inawafanya kutokuwa na uhakika wa ajira zao na hata kupata malipo duni kama ilivyoeleza kwenye ripoti hiyo licha ya kuchangia ajira kwa vijana wanaochangia kwenye pato la Taifa kwa kulipa kodi.
Ripoti hiyo ni matokeo ya awamu ya pili ya utafiti yaliyotolewa leo Oktoba 20 jijini hapa na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa) uliolenga kuangalia namna sera na sheria zinavyoweza kufanya kazi katika sekta hiyo inayohusisha watoa huduma za teksi mtandao.
Awamu ya kwanza ya utafiti uliofanyika mwaka jana ulionyesha kuwa maelfu ya watu nchini Tanzania wanafanya kazi katika uchumi wa kidijitali ikiwemo kutoa huduma za taksi mtandao lakini huenda wafanyakazi wakakabiliwa na malipo duni na mazingira hatarishi.
Kufuatia hilo utafiti huo umependekeza watunga sera na wadau kuungana kushughulikia hali mbaya ya kazi katika eneo hilo la biashara ya mtandao.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, mtafiti mkuu katika utafiti huo Hilda Mwakatumbula amesema uchumi wa jukwaa la Afrika unatabiriwa kujumuisha zaidi ya wafanyakazi milioni 80 ifikapo mwaka 2030 na hivyo ni muhimu mazingira bora yatengenezwe kuhakikisha inakuwa chanzo kimoja wapo cha ajira.
Alisema Serikali inapaswa kufafanua kwa uwazi haki na wajibu husika wa mfanyakazi wa jukwaa analofanyia kazi kwa kuweka vigezo vinavyohakikisha ulinzi na manufaa ya pande zote mbili.
"Serikali inahitaji kuharakisha juhudi za kusajili rasmi wafanyakazi wa jukwaa na kuhitaji utoaji wa bima ya afya, majukwaa yanapaswa kuchangia asilimia fulani kulingana na kiasi kinacholingana na muda wa kazi au mapato ya jukwaa husika," alisisitiza.
Akizindua ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibi wa Usafiri wa Ardhini (Latra), Habib Suluo amesema utafiti huo umekuja wakati muafaka ambapo mamlaka inajiandaa kukutana na wadau kwenye jukwaa hili ili kujua changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua kwa pamoja.
Suluo ametumia fursa hiyo kuwataka madereva wanaojihusisha na huduma za taksi mtandao kuwa waaminifu na kaucha kuhujumu mifumo.
“Hii ni kinyume na taratibu zetu, tumeshaona mifumo yetu iko imara na tunaifanyia kazi, tunataka watu walioamua kuingia kwenye biashara hii wawe wakweli maana jukwaa hili linakuwa kwa kasi na litakuwa kimbilio kwa wananchi wengi katika siku za usoni
“Binafsi nilikutana na changamoto hii, nikapanda kutoka Uwanja wa Ndege, dereva akanilazimisha kukatisha safari ili nimpe pesa taslimu bila mfumo kutambua, nikakataa,” amesema Suluo.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Mtandaoni Tanzania (Toda), Neema Mushi amesema tangu kuanza kufanyika kwa utafiti huo, kwa kiasi fulani kampuni za teksi mtandao zimeanza kubadilika na kuwajali madereva wao.
Ameongeza kuwa hata kwa kampuni mpya zinazoanza biashara nchini, zimeanza kuzingatia sheria na taratibu, ikiwamo kuweka mazingira rafiki kwa madereva na kukaa na madereva na kusikiliza kero zao.
“Lakini bado kuna changamoto baadhi ya kampuni za zamani kutozingatia sheria na matokeo yake hata hizi kampuni mapya zinaiga yale yanayofanywa na waliowatangulia na kuwaumiza madereva, kwa mfano jinsi ya kulipia safari kwa kilomita moja inayosababisha makato makubwa.
“Kuna changamoto nyingi katika biashara hii kama vile kutokuwa na mikataba ya ajira, bima ya afya dereva akipata ajali anajihudumia na utafiti huu utasaidia kufungua milango ya mazungumzo ili vijana wapate haki zao,” ameongeza Neema.
Kuhusu madai hayo Neema amekiri kuwepo kwa madereva wanaofanya hivyo akieleza kusukumwa na tozo za wamiliki wa majukwaa hayo ni kubwa hivyo kuondoa uwezekano wa dereva kupata faida.