Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania, Dk Stella Bitanyi amesema asilimia 65 ya vifo vya ng'ombe vinasababishwa na mdudu kupe (ndorobo).
Amesema mdudu huyo anayesababisha magonjwa makuu mawili, asilimia 80 kati ya vifo hivyo vinatokana na aina ya ugonjwa wa ndigana kali ukilinganisha na ndigana baridi.
Dk Stella ameyasema hayo jana Ijumaa Oktoba 21, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na mwelekeo wa bajeti wa Maabara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2022/23.
Amesema ugonjwa huo unaongoza kuua ng'ombe na ni gharama zaidi katika matibabu yake.
"Magonjwa yote ya wanyama yanaua ila inategemea yametokea kwa kipindi gani kwasababu Kuna magonjwa ya mlipuko ambayo huua Kwa kasi Kwa wakati mmoja na wapi lakini huu ugonjwa upo siku zote na unaathiri sana na una gharama katika matibabu yake," amesema.
Kufuatia vifo hivyo Dk Stella amesema Wizara ipo katika mpango wa kuhakikisha kuwa kila kata na kijiji kinakuwa na josho na kutoa dawa za kuogeshea mifugo zinazotokana na ruzuku kutoka Serikalini.
Dk Stella amesema tangu Maabara hiyo ipewe mamlaka na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutafiti na kuzalisha chanjo, chanjo 65 milioni za mifugo kama ng'ombe, kuku, kondoo, mbuzi na mbwa zimezalishwa.