Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utafiti: Biashara chache za wanawake zinaomba zabuni Serikalini

Pic Fedha Data Wastaafu Utafiti: Biashara chache za wanawake zinaomba zabuni Serikalini

Sun, 25 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakati wafanyabiashara wanawake wakionekana kutochangamkia zabuni zitolewazo na Serikali, utafiti umeonyesha ugumu wa kupata taarifa sahihi na utaratibu unaohusu zabani hizo, watajwa kuwa chanzo wengi kutonufaika fursa hizo.

Hayo yamebainishwa katika utafiti uliopewa jina la: “Kuelekea Usawa wa Kijinsia: Kuelewa vikwazo na suluhisho la biashara zinazoongozwa na wanawake Afrika Mashariki (Tanzania).” ambao kwa Tanzania umefanywa na Taasisi ya The Chanzo Initiative kwa kushirikiana na Africa Freedom of Information Centre (AFIC). Kwa mujibu wa utafiti huo, jumla ya biashara 23 zinazoongozwa na wanawake zimewahi kutuma maombi ya zabuni Serikalini huku biashara 36 zikiwa hazijawahi kutuma maombi hayo.

Utafiti huo unaeleza kuwa biashara zinazoongozwa na wanawake ni asilimia 48.1 ya biashara zote nchini, ambapo biashara nyingi za wanawake zinazofanya biashara ya jumla ni takribani asilimia 60 ya biashara hizo.

Utafiti huo umeendelea kubainisha kuwa katika biashara za huduma, asilimia 26 zinaongozwa na wanawake, wakati kwenye sekta ya viwanda, wanawake wanachukua 11 ya biashara ahizo na kwamba asilimia 3 ya biashara za wananawake ziko katika sekta nyinginezo.

Washiriki katika utafiti huo waliulizwa kwanini hawakuwahi kuwasilisha maombi ya zabuni yoyote Serikalini, wengi wao walijibu kuwa ni kwa sababu ya ugumu wa kupata habari sahihi, na kwa wakati sahihi kuhusu fursa hizo na kutojua utaratibu wake.

“…hii ilitokana na ugumu wa upatikanaji wa taarifa muhimu na kwa wakati kuhusu fursa na taratibu za zabuni hizo, lakini pia ugumu wa kukidhi mahitaji muhimu ya zabuni pamoja na kutopata fedha/mikopo ya kuwekeza kwenye biashara,” inasomeka sehemu ya utafiti huo.

Hata hivyo Mtafiti kutoka Taasisi ya The Chanzo Initiative, Joel Ntile amesema walibaini changamoto kubwa miongoni mwa wanawake, ni mtazamo hasi, ‘kwamba, ili kushinda zabuni za Serikali, unahitaji kuhonga baadhi ya watu katika mchakato huo.’

Mtafiti Ntile amebainisha kuwa katika utafiti huo, wamegundua suala la mitaji kuwa changamoto nyingine kwa biashara hizo.

“…suala la mtaji kwa wanawake wengi nchini ni changamoto, wanawake wengi wanakosa misuli ya kushindana na wanaume katika kupata zabuni za Serikali,” amesema na kuongeza.

“Ni vema Serikali ikaangalia namna bora ya kuunganisha mikopo inayotolewa kwa wanawake na zabuni za Serikali. Kwa maneno mengine, wanawake wanaopata mikopo ile asilimia 10 toka halimashauri, basi wapewe kipaumbele wakati wa mchakato wa zabuni ili kuwawezesha kukuza biashara zao na kurejesha mikopo hiyo.” Kwa upande wake, Mratibu wa Tathmini na Uchambuzi kutoka AFIC, Charity Komujjurizi anadhani kuna umuhimu kwa Serikali kubadilisha mfumo wa utoaji mikopo ya asilimia 30, akisema zitolewe kwa biashara za mwanamke mmoja mmoja na siyo kwa kikundi kama inavyoelezwa kwenye sheria. “Uundwaji wa vikundi ili kukidhi matakwa ya sheria ya manunuzi ni changamoto mojawapo kwa wanawake, kwani wanatakiwa kutafutana ili kufanya kazi kwa pamoja. Nadhani biashara za mwanamke mmoja mmoja zilizofanikiwa zipewe mikopo ili kufaidika bila kusubiri makundi,” amesema Charity.

Chanzo: Mwananchi