Vyama vya Ushirika mkoani Mtwara vimemuomba Mkuu wa mkoa huo kuvishika mkono dhidi ya wanaovipiga mawe wakiwa na lengo la kuvigawa.
Kimsingi Mkoa wa Mtwara una vyama vya ushirika 417 vikiwemo vikuu viwili ambavyo ni Chama cha Ushirika Masasi, Mtwara (MAMCU) na Chama cha Ushirika Tandahimba Newala (TANECU). Inadaiwa kuwa, kwa pamoja, vyama vyote vinasimamia wanachama 115,679 na mali zenye thamani ya Sh18.7 bilioni.
Mwenyekiti wa vyama vya ushirika mkoani hapa ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa TANECU, Karim Chipola amesema leo Ijumaa Juni 2, 2023 katika Jukwaa la maendeleo ya ushirika kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kukosa uhuru wa kufanya kazi za ushirika.
Changamoto hii amesema imetoka kwa baadhi ya watu wasioutakia mema ushirika kushawishi mgawanyiko wa vyama vya MAMCU na TANECU kwa dhamira za malengo yao binafsi.
"Ushirika huu ndio unaofanya kuwe na utulivu kwa kusimamia rasilimali fedha za wananchi vinginevyo kungekuwepo na vurugu ambazo zingefika hadi kwa viongozi wa juu. Tukuombe uwashike mkono viongozi wa ushirika na kuulinda ushirika kwani ndio kimbilio la wanyonge,” amesema Chipola.
Mrajisi Msaidizi wa Mkoa, Ibrahim Kakozi amesema kuwa katika msimu uliopita 2022/2023 vyama vya ushirika vimekusanya na kuuza korosho tani 93 zenye thamani ya Sh174.8 bilioni na ufuta tani 9 wenye thamani ya Sh28.9 bilioni.
Aidha Mrajisi amesema kiasi cha Sh203.7 bilioni kimepita kwenye akaunti mbali mbali za vyama vya ushirika katika mkoa wa Mtwara kwenda kwa wadau mbali mbali.
Amesema miongoni mwa changamoto za ushirika mkoani hapa ni baadhi ya wadau kuwashawishi wakulima kuanzisha vyama vipya vya msingi.
Kwa upande wa Francis Alfred Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho nchini (CBT), amesema iwapo wana ushirika wataongea lugha moja kwa nia ya kuinua uchumi hakuna ambalo litashindikama.