Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafirishaji vifurushi waibua pande mbili

45705 Pic+usafirishaji Usafirishaji vifurushi waibua pande mbili

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Pande mbili zimejitokeza zikitofautiana katika suala la usafirishaji vifurushi kufuatia kauli ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye aliyeagiza watoaji wa huduma hiyo kuwa na vibali na leseni.

Kati ya pande hizo, wapo waliounga mkono huku wakisema ukubwa wa utoaji wa huduma hiyo unatofautiana kati ya kampuni moja ya usafirishaji na nyingine na hivyo kushauri bei elekezi zizingatie hilo, huku wengine wakidai hakuna haja ya kuwa na leseni wala vibali.

Kauli hizo zimekuja baada ya naibu waziri huyo kutoa tamko Machi 5 akiwa mkoani Mara alikozungumza na watendaji na watumishi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Nditiye aliipa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (Sumatra) wiki mbili kufanya ukaguzi wa mabasi kama yana leseni na vibali vya kusafirisha vifurushi.

Wakizungumza na Mwananchi, wadau waliounga mkono walisema ni jambo jema mabasi kukata leseni zitakazosaidia kuwepo kwa utaratibu wa kusafirisha vifurushi tofauti na ilivyo sasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Hassan Mchanjama alisema kwa sasa gharama za kusafirisha vifurushi zimekuwa kubwa tofauti na uhalisia, lakini kutumika kwa sheria kutakuwa na mfumo mzuri.

“Sasa hivi kima cha chini kusafirisha kifurushi cha bahasha ndogo ni Sh5,000, ni gharama kubwa ninaona. Ninaomba Serikali iweke bei elekezi ya kukata leseni ili kupunguza mzigo wa watu wanaotaka kusafirisha vifurushi,” alisema Mchanjama.

“Kwa jinsi nilivyoona gharama za kukata leseni au kibali kwa ajili ya mchakato ni kubwa na zitawaweka katika wakati mgumu wanaotaka kusafirisha vifurushi vyao, (maana) wenye mabasi watakaopata leseni lazima watafidia gharama zao kwa wanaotaka kusafirisha vifurushi.”

Wakala wa mabasi ya HG, Athuman Makuka aliungana na Serikali kuhusu mchakato huo, lakini akaomba mamlaka husika kuwaangalia zaidi wenye mabasi mengi ambao husafirisha mara kwa mara vifurushi.

“Kuna mabasi sitaki kuyataja ndiyo yanafanya biashara ya kusafirisha vifurushi kila siku tofauti na magari mengine, lakini mabasi mengi ni nadra kusafirisha vifurushi hivi. Je, ni halali kukata hii leseni wakati unapata tenda hii kwa manati tofauti na wenzako. Serikali itufikirie kwa hili,” alisema Makuka.

Hata hivyo, abiria aliyekuwa katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo jana, Happiness Paul alisema sheria ya usafirishaji vifurushi ni nzuri, lakini ni vyema utekelezaji wake ukazingatia pande zote.

Alisema kwa kuangalia watakaoathirika ni wale wanaotaka huduma ya kusafirisha vifurushi kwa kuwa wataongezewa gharama.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu alisema mwaka huu ni wa maumivu kwao hasa katika sekta ya usafirishaji, akisema chama chao hakikushirikishwa katika mchakato wa sheria hiyo.

“Sasa hivi hali ni ngumu katika sekta hii, unaposema wenye mabasi wakate leseni unatuweka katika njia panda. Hizi fedha kidogo tunazopata kutokana na vifurushi zinatusaidia kuziba pengo la abiria na kununua mafuta kidogo, sasa tunakata leseni hatutapa kitu hapo,” alisema Mrutu.



Chanzo: mwananchi.co.tz