Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafirishaji bidhaa nje kuboreshwa

EXPO Usafirishaji bidhaa nje kuboreshwa

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe, amewaahidi wasafi rishaji wa bidhaa nje ya nchi kuwa, serikali itashughulikia mapendekezo yao na changamoto zinazowakabili ili wafanye biashara kwa ufanisi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika kikao kilichowakutanisha wadau wa usafirishaji bidhaa nje na watendaji wa serikali, Profesa Shemdoe alisema serikali inatambua changamoto wanazokutana nazo.

“Niseme wazi kuwa haya mliyoyapendekeza ninayachukua na nina waahidi kuyapeleka sehemu husika na yatapatiwa ufumbuzi,” alisema.

Aliwaomba wasafirishaji bidhaa nje ambao ni wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kuandaa vikao vya majidiliano walau mara nne kwa mwaka.

“Naomba muwe mnaandaa vikao hivi walau mara nne kwa mwaka. Vikao hivi vitatupa dira sahihi ya kujua wapi tunakwenda na wapi tunakwama ili pafanyiwe marekebisho,” alisema Profesa Shemdoe.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Zachy Mbenna, alimshukuru Profesa Shemdoe kwa kushiriki katika kikao hicho na kueleza kuwa, taasisi hiyo inaridhishwa na uhusiano kati yake na serikali.

“Kwa namna ya pekee naipongeza sana serikali kwa namna wanavyoshirikiana na sisi na niseme wazi kuwa sisi tuko nyuma ya serikali kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unazidi kuimarika,” alisema Mbenna.

Aliwataka wasafirishaji wa bidhaa nje wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa zilizopo ndani na nje ya ili kuiingiza fedha ya kigeni.

“Nchi yetu inaingiza fedha nyingi za kigeni kupitia sekta hii ya usafirishaji bidhaa nje ya nchi, sasa nitoe rai kwa wadau mjitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii ili serikali ipate mapato na wasafirishaji wapate mapato,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, alisifu ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi na kuiomba serikali kuzibadilisha sera na sheria zinazokwamisha usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.

“Ni wazi Serikali ya Rais John Magufuli inajitoa sana kushirikiana na sekta binafsi, hili ni jambo la kuvutia sana kwani maendeleo ya nchi yoyote muhimu kuhusisha sekta binafsi,” alisema Kirenga na kuongeza:

“Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na serikali, ombi langu kubwa sasa ni hizi sera na sheria zinazotukwamisha sekta hii zipitiwe nazifanyiwe maboresho ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.”

Chanzo: habarileo.co.tz