Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri wa anga Afrika ni ghali kuliko sehemu yoyote duniani

Ndege Yarejea Usafiri wa anga Afrika ni ghali kuliko sehemu yoyote duniani

Tue, 11 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mara nyingi ni rahisi kusafiri bara moja hadi jingine, kuliko kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine ndani ya Afrika.

Kwa ulinganisho wa haraka, kusafiri kutoka mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, hadi jiji kubwa la Uturuki, Istanbul, huenda ikakugharimu dola za kimarekani 150, kwa safari ya moja kwa moja ya ndege ya chini ya saa tatu.

Lakini kwa kuruka umbali kama huo, mfano kati ya Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na jiji kubwa la Nigeria, Lagos, utalipa kati ya dola za kimarekani 500 na 850, na mutasimama angalau mara moja na safari inachukua hadi saa 20.

Hii inafanya biashara ndani ya Afrika kuwa ngumu sana, na ya gharama kubwa.

Shirikisho la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) - linalowakilisha baadhi ya mashirika 300 ya ndege ambayo yanaunda takriban 83% ya usafiri wa anga duniani – linasema, ikiwa nchi 12 tu barani Afrika zitafanya kazi pamoja kuboresha mawasiliano na kufungua masoko yao, nafasi za kazi 155,000 zitaundwa na kukuza pato la taifa la nchi hizo kwa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1.3.

"Usafiri wa anga unachangia moja kwa moja pato la taifa katika kila nchi. Unazalisha kazi na kuchochea kukua kwa uchumi," anasema Kamil al-Awadhi, makamu wa rais wa IATA, Afrika na Mashariki ya Kati.

Profesa msaidizi wa sheria za kibiashara katika Chuo Kikuu cha Durham cha Uingereza, Adefolake Adeyeye, anakubali kwamba Afŕika kwa ujumla inapata hasara kutokana na huduma yake duni ya anga.

"Usafiri wa anga unakuza uchumi. Kama tulivyoona katika mabara mengine, mashirika ya ndege ya ya bei rahisi yanaweza kuboresha mawasiliano na gharama, na kupelekea kukuza utalii, ambao unazalisha ajira nyingi zaidi," anasema.

Karibu 18% ya watu duniani wanaishi barani Afrika, ni 2% ya tu ya safari za anga duniani zinafanyika barani humo, kulingana na ripoti ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa. Vilevile ni 3.8% tu ya uzalishaji wa gesi chafu duniani hufanyika Afrika. Hii ni tofauti na 19% kutoka Marekani na 23% kutoka China.

Afrika ina utajiri wa madini na maliasili, lakini kati ya mataifa 46 kwenye orodha ya Umoja wa Mataifa ya mataifa yenye maendeleo duni, 33 yapo barani Afrika. Huku umaskini ukiendelea kuwa tishio kubwa la kila siku kwa mamilioni ya watu barani humo.

Lakini pia kuna watu wa tabaka la kati wenye uchumi mzuri, ambao wanaweza kusafiri kwa ndege ikiwa tiketi zingeuzwa kwa viwango sawa na Ulaya au kwingineko.

Mataifa ya Afrika yamekuwa yakijaribu kwa miongo kadhaa kuunganisha sekta ya usafiri wa anga, lakini bado hayajafanikiwa.

Afrika inakwama wapi?

"Kuna haja ya kuwa na mkakati madhubuti wa Afrika kushughulikia suala la huduma yake duni ya anga kama wanataka kubadilisha uchumi wa Afrika," anasema Zemedeneh Negatu, mwenyekiti wa kampuni ya uwekezaji yenye makao makuu nchini Marekani ya Fairfax Africa Fund.

Anasema, safari za ndege ndani ya Afrika bado zimeundwa kwa makubaliano magumu kati ya nchi moja na nchi nyingine, na mashirika mengi ya ndege ya kiserikali yanajiendesha kwa shida, huku mengine yakipata hasara.

"Kila serikali barani Afrika inataka kuona bendera yake kwenye mkia wa ndege katika uwanja wa ndege wa Heathrow au uwanja wa ndege wa JFK, lakini serikali za Afrika zinapaswa kutambua kwamba kila nchi kujisimamia pekee ni jambo lisilo wezekana."

Zemedeneh anasema, mashirika ya ndege ya Kiafrika yanapaswa kuiga kutoka Ulaya na kuunda ushirikiano wao, kama ushirikiano wa Air France na KLM ya Uholanzi, na Kundi la Ndege la Kimataifa la Anglo-Spanish (IAG) lililoundwa kwa ushirkiano wa British Airways na Iberia.

Anasema hata katika soko tajiri la Ulaya, msongamano ni njia pekee kwa ndege kuishi, na kutoa huduma ya bei nafuu zaidi na ya kutegemewa.

Mfumo wa sasa barani Afrika umegawanyika sana, ingawa nchi 35 zimetia saini kwenye Soko Moja la Usafiri wa Anga la Afrika, mpango wa Umoja wa Afrika (AU) wa kuweka soko huru la anga na kupunguza gharama, inaweza kuchukua miaka kabla ya kutekelezwa.

Bw Awadhi wa IATA anasema serikali zinasitasita kufanya kazi pamoja, "kuna ugumu ambapo kila nchi hufikiri inajua jinsi ya kushughulikia vizuri zaidi na kushikilia mbinu hata kama hazifanyi kazi," anasema.

Kuna mashirika machache barani Afrika ambayo yamestawi, na yanaweza kutoa mwongozo kwa mashirika mengine - mfano Ethiopian Airlines. Zaidi ya miaka 15 iliyopita kampuni hiyo iliajiri watu wapatao 4,000. Sasa idadi hiyo ni zaidi ya 17,000. Inamilikiwa na serikali lakini inaendeshwa kama mradi wa kibiashara bila kuingiliwa na serikali.

Imeongeza zaidi ya mara mbili uwezo wake wa kuchukua mizigo na abiria na imeifanya Addis Ababa kuwa uwanja mkubwa wa kikanda, ikiingiza fedha za kigeni katika mji mkuu wa Ethiopia, na kukuza sekta ya huduma nchini humo.

Mwanzoni mwa milenia Ethiopia ilikuwa mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, sasa ni mojawapo ya nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi.

Bw Zemedeneh, raia wa Ethiopia mwenye asili ya Marekani ambaye alichukua jukumu muhimu kama mshauri wa Shirika la Ndege la Ethiopia anasema shirika hilo limetoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi.

"Shirika la ndege la Ethiopia linazalisha mamilioni ya dola kwa ajili ya nchi, na linamfanya kila Muethiopia ajivunie kwamba wameweza kuunda mojawapo ya makampuni ya kimataifa yenye mafanikio makubwa yanayomilikiwa na Waafrika, yanayoendeshwa na Waafrika," anaongeza.

Wasafiri wa Kiafrika watakuwa na matumaini kwamba aina hii ya mafanikio ya kibiashara yatawafikia na wao na hatimaye waweze kufika wanakotaka kwenda kwa haraka na kwa bei nafuu zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live