Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri mikoani wadorora Ubungo

85332cbeb7d5bc455c76e969e515495b Usafiri mikoani wadorora Ubungo

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUCHELEWA kufungwa kwa shule, kumechangia kuiathiri sekta ya usafiri wa mabasi, hususani katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kutokana na mabasi mengi kusafiri na abiria wachache, ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Akizungumza na HabariLEO jana, Naibu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), John Mbazi alisema hali hiyo imesababisha uwepo wa idadi ndogo ya abiria hususani wanaosafiri kutumia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT).

“Ukweli ni kwamba kuchelewa kufungwa kwa shule mara baada ya utaratibu wa Wizara ya Elimu tangu kumalizika kwa ugonjwa wa Covid 19, kumesababisha kupungua kwa idadi ya abiria, hii inatokana na kuwa wazazi wengi hawawezi kusafiri bila watoto wao,”alisema.

Alisema matarajio yao hali hiyo kituoni inaweza kubadilika kuanzia wiki ijayo mara baada ya shule mbalimbali kufungwa kuanzia kesho, jambo linaloweza kuwafanya wazazi wengi kuanza kupanga safari zao, hivyo kuamsha upya hali ya usafiri kituoni hapo.

Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Taboa, Mustafa Mwalongo alisema hadi sasa usafiri wa mabasi hususani katika kituo hicho cha Ubungo, hauna changamoto zozote zilizokuwa kipindi kama hiki miaka ya nyuma, kiasi cha kuwafanya watu kupata taabu ya usafiri.

Aidha, alisema kwa kuwa zimesalia siku chake kuelekea sikukuu, matarajio yao huenda hali hiyo itabadilika. Aliwataka wananchi wote wanaotarajia kusafiri kwa ajili ya sikukuu hizo, kukata tiketi zao mapema ili kuepuka usumbufu.

“Ukweli mwaka huu umekuwa wa tofauti sana na huko nyuma, abiria bado ni wachache kiasi cha kusababisha hata baadhi ya mabasi kuamua kusitisha safari zake kwa kukosa abiria, imani yetu pengine hali inaweza kubadilika kuanzia wiki ijayo,”alisema.

Alisema miaka ya nyuma nyakati kama hizi, kituo cha mabasi cha Ubungo na vinginevyo mikoani, hutawaliwa na pilika za abiria wengi kutaka usafiri kwenda mikoani, hususan mikoa ya Kaskazini, kwa ajili ya kusheherekea na ndugu zao sikukuu za mwisho wa mwaka.

Chanzo: habarileo.co.tz