Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri mikoani janga

035be1a6689c82851967510e3dfe3372.png Usafiri mikoani janga

Thu, 24 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI kesho Watanzania wanaungana na watu wengine duniani kusherehea sikukuu ya Krismasi, hali ya usafiri wa kwenda mikoani imekuwa ni janga kutokana na mlundikano wa abiria huku kukiwa hakuna magari ya kutosha.

HabariLEO lilishuhudia umati mkubwa wa abiria katika kituo cha mabasi ya mikoani cha Ubungo wakiwa hawajui la kufanya baada ya kusota kituoni hapo kwa muda mrefu bila kuwa na matumaini ya kusafiri huku wakiambiwa kuwa mabasi yamejaa kuanzia jana hadi leo.

Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) tayari imetoa jumla ya vibali 41 kwa magari yenye ruti tofauti kusafirisha abiria hao wa mikoani ili kupunguza adha hiyo ya uhaba wa magari ya kwenda mikoani.

Akizungumza na gazeti hili, Janet Msangi alieleza kuwa alifika kituoni hapo tangu alfajiri kwa matumaini ya kupata usafiri wa kwenda Moshi Kilimanjaro lakini alikuta hali ni mbaya kutokana na wingi wa watu huku magari mengi yaliyokuwepo kituoni hapo yakiwa yamejaa.

“Kama unavyoona watu ni wengi hakuna hata pa kukanyaga, magari hakuna lakini pia nauli zimepanda kuliko kawaida, tunaomba mamlaka zitusaidie,” alieleza.

Edna Mwakalinga, aliyekuwa akisafirisha mtoto wake kwenda mkoani Iringa alisema pamoja na kwamba alikuwa tayari na tiketi lakini alishangazwa na umati mkubwa wa watu kituoni hapo.

“Nimekuja hapa tangu saa 11.30 alfajiri ili mwanangu apande basi la saa 12 lakini hali niliyoikuta ni mbaya yaani ukikaa vibaya unampoteza mtoto ilibidi nimwambia anishike nguo yangu ili tusipoteane. Nashukuru nilikata tiketi mapema,” alisema.

Mmoja wa abiria Japhet Kimaro alilalamika kupandishiwa nauli kuliko bei ya kawaida ambapo nauli ya kwenda Moshi kwa basi alilotakiwa kupanda ambalo hata hivyo tiketi yake haikuonyesha ni basi gani ilikuwa 32,000 lakini alilipa Sh 50,000.

“Wapo wengine hapa wamelipa leo hadi Sh 70,000 ili tu waondoke. Mimi bado nasubiri hilo basi Mungu tu anisaidie,” alisema.

Uchunguzi uliofanywa na Habari LEO unaonyesha kuwa, kujaa kwa mabasi hayo kunachangiwa na wapiga debe na madalali ambao wanazinunua tiketi hizo ama kukubaliana na mawakala wa mabasi hayo kuziuza kwa bei ya juu bila kumshirikisha mmiliki.

Siku ya juzi abiria waliopanda gari ya Massama linalofanya safari za Dar es salaam na Arusha walitozwa kati ya Sh 30,000 hadi Sh 50,000 kutegemeana na dalali aliyemuuzia.

Bei halisi ya basi hilo ni Sh 23,000 lakini wafanyabiashara hao wamewatoza abiria fedha nyingi huku madalali hao wakiwaeleza kuwa endapo mtaulizwa wamekata shilingi ngapi waseme ni Sh 23,000.

"Hebu tukubaliane. Wewe una pesa au una nauli? Kama unahitaji usafiri unifuate nauli halali ni Sh 23,000 lakini tunauza kwa Sh 45,000. Usije kugeuka baadae na nauli yako itaandikwa Sh. 23,000,"alisema mmoja wa madalali.

Kwa upande mwingine majira ya saa 11 alfajiri daladala tatu zilizokuwa eneo la kituo cha mafuta cha Ubungo zilikuwa zimejaza abiria wanaokwenda mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambao walitozwa kati ya Sh 45000 na Sh 50000.

Hali ilivyokuwa jana abiria walifurika kituo hicho cha mafuta pamoja na stendi ya Ubungo na hivyo kuzuia biashara ya mafuta. Pamoja na hayo wingi wa watu katika kituo kile ni hatari kwa usalama wao wenyewe.

Kwa upande wa mkoa wa Dodoma hali ya usafiri kwa mabasi ya mkoani ilikuwa tete pia kwani watu wengi walijaa kwenye stendi kuu ya mabasi wakiwa hawajui hatma ya safari zao.

Lakini pia abiria wengine walijazana kando ya barabara ya kwenda Dar es Salaam nje ya stendi, eneo la CBE na Four ways wakijaribu kutafuta usafiri binafsi kwa ajili ya safari zao.

HabariLEO ilishuhudia magari binafsi ya aina mbalimbali zikiwamo Noah zikisafirisha abiria kutoa Dodoma kwenda maeneo mbalimbali huku wanaokwenda Dar es Salaam wengine wakilazimika kuunganisha hadi Morogoro kwa imani ya kupata mabasi yanayoanza mkoani humo.

"Shida kubwa iko kwenye mabasi ya kwenda kaskazini ya kwenda Dar angalau mabasi yanayotoka Mwanza au Tabora, na tunawapandish abiria wawili au watatu, na hali ya ugumu wa safari imeanza tangu wiki iliyopita," alisema wakala wa kukata tiketi Stendi kuu Richard Joseph.

Mabasi mwengi yanayoanzia safari zake mkoani hapa yamejaa na nafasi inapatikana kuanzia Desemba 28 huku bei ya nauli ikiwa ile ile kwa wale wanaokata tiketi zao kwenye ofisi za kampuni za usafirishaji.

Ofisa Uhusiano wa LATRA, Salum Pazi katika kushughulikia kadhia hiyo, alisema mamlaka hiyo imeweka kikosi maalumu katika stendi hiyo ya Ubungo kwa ajili ya kufuatilia na kushughulikia mwenendo wa usafiri.

Alisema kazi kubwa ya kikosi hicho ni kutoa vibali papo hapo kwa magari yenye ruti tofauti ili kuongeza nguvu katika maeneo yenye uhitaji zaidi wa abiria lakini pia kudhibiti upandishwaji holela wa nauli.

“Hata hivyo, tuna changamoto kubwa ya kutopata ushirikiano mzuri kutoka kwa abiria kwani wanazidishiwa gharama za nauli kuliko zile halali na kukubali kuandikiwa nauli halali kwenye tiketi hali inayokuwa vigumu kuwakamata wahusika,” alisema Pazi.

Alisema kikosi hicho kinaendelea kudhibiti na kuchunguza matukio hayo ya uzidishaji nauli na kuwataka abiria wakipe ushirikiano kwani wanaokamatwa na kuthibitika kufanya kosa hilo huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia usafiri wa reli kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) alisema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na shirika hilo pia wamechukua hatua za kuhakikisha wanapunguza msongamano wa abiria waaohitaji usafiri kwa kuongeza ruti za treni.

“Awali kulikuwa na treni nne kwa wiki zinazokwenda mikoa ya Kaskazini taani Tanga, Kilimanjaro na Arusha kutokea Dar es Salaam sasa hivi zimeongezwa na kufikia treni sita,” alisema.

Alisema pia uwezo wa treni hizo wa kubeba abiria nao umeongezwa kutoka abiria 600 hadi kufikia abiria 1,000.

Habari hii imeandikwa na Halima Mlacha, Lucy Ngowi Dar na Anastazia Anyimike Dodoma

Chanzo: habarileo.co.tz