SERIKALI imesema kuwa uzalishaji na matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini ndio njia pekee ambayo itasaidia kukuza uchumi na kupunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Tanga, Arbogast Kimasa wakati wa ufungaji wa warsha ya kukuza ujuzi kwa wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za kusindika mkoani hapa.
Alisema kuwa serikali inahitaji kupunguza matumizi ya fedha za kigeni lakini na kuongeza matumizi ya malighafi kwenye viwanda vyetu wenyewe ndio maana imekuwa ikitia msisitizo wa kuendelea kuwajengea uwezo wananchi.
“Niwaombe washiriki wa mafunzo haya kutumia vizuri fursa zinazopatikana katika Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo SIDO ili kuhakikisha kuwa viwanda mtakavyoanzisha vinazalisha bidhaa zenye ubora na kukidhi hitaji la soko la ndani ya mkoa na Tanzania kwa ujumla,” alisema Kimasa.
Aidha aliwataka watendajj wa halimashauri kufuatilia maendeleo ya wanufaika wa mafunzo ikiwemo kuwajengea uwezo wa fursa za mikopo kwenye maeneo yao ili waweze kukuza biashara zao na kuweza kujiajiri na kuajiri wenzao.
Kaimu Meneja wa SIDO mkoa wa Tanga Liberat Macha ambao ndio waratibu wa mafunzo hayo kwa kushirikiana na na Mamlaka ya elimu Tanzania TEA alisema kuwa wanatarajia kuendesha mafunzo hayo kwa vijana 400 mkoani hapa.
Alisema vijana hao wamepewa mbinu mbalimbali za kuongeza ujuzi na thamani ya mazao yao sambamba na kuongeza fursa za ajira hasa katika kipindi hiki ambacho ajira za serikali zimekuwa haba.
Mmoja wa wanufaika hao Maria Mavoa alisema kuwa kabla ya mafunzo alikuwa anazalisha bidhaa ambazo zilikuwa zinaharibika baada ya siku mbili lakini kwa elimu waliyoipata ameweza kujua mbinu ya kufanya bidhaa zake kudumu.