Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ununuzi vifaatiba nje ya nchi unavyoongeza gharama za matibabu

WhatsApp Image 2022 07 17 At 1.jpeg Ununuzi vifaatiba nje ya nchi unavyoongeza gharama za matibabu

Tue, 31 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uagizaji wa vifaatiba nje ya nchi na magonjwa yasiyoambukiza, vimetajwa kuwa sababu ya ongezeko la gharama huduma za afya kwenye kaya.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Kufuatilia Kaya (NPS) ya mwaka 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kuna ongezeko la gharama wanazotumia wanakaya kupata huduma za afya kwa mwaka ikilinganishwa na ilivyokuwa 2014/2015.

Ripoti imebaini waliotumia chini ya Sh10,000 katika kipindi cha wiki nne kabla ya utafiti walikuwa asilimia 66.9 wakati waliotumia kiasi kama hicho miaka sita iliyopita ni asilimia 80.5.

Waliotumia kiasi cha zaidi ya Sh10,000 walikuwa asilimia 33.1 mwaka 2020/21 ukilinganisha na asilimia 19.5 waliofanya matumizi kama hayo mwaka 2014/2015.

Wadau wa afya wamesema, suluhisho la wananchi kutotumia fedha nyingi wanapokwenda hospitali ni kuwa na bima ya afya itakayomwezesha kupata huduma bila kutoa fedha mfukoni.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, Alex Ernest alisema ongezeko la gharama limechangiwa na magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, shinikizo la juu la damu, kisukari na matatizo ya figo.

“Magonjwa haya sugu yameongeza matumizi ya fedha katika huduma za afya hivi karibuni, hata hivyo wananchi wengi wanapata changamoto ya mwendelezo wa matibabu kwa kukosa fedha, hivyo bima ya afya kwa wote itakuwa mkombozi,” alisema Dk Ernest.

Mtaalamu wa Maabara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Alex Mlwisa alisema kuongezeka kwa gharama za huduma za afya kunasababishwa na gharama za vifaatiba na uendeshaji.

“Suluhisho kwa upande wa vifaa tiba ni kuwekeza ujuzi kwa Watanzania, vifaa tiba hivi vizalishwe hapa nchini. Nashauri NBS kuangalia uhalisia wa gharama za afya, nimekuwa nikiwapeleka watoto hata mimi mwenyewe kutibiwa, gharama ni kubwa zaidi ya Sh30,000 na hii ni kwa ajili ya kumuona daktari, vipimo pamoja na dawa,” alisema.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi alisema ongezeko la gharama za watu kupata huduma za afya kulingana na takwimu za NPS lipo.

“Lakini pia ongezeko la takwimu hizo zinaweza kuchangiwa na masuala ya kiuchumi, thamani ya dola mwaka 2014/15 na mwaka 2020/21 ni tofauti, nayo inaweza kuwa sababu, nayo magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameongezeka,” alisema.

Sophia Peter, mkazi wa Temeke alisema ongezeko la matumizi ya wananchi kwenye huduma za afya kumechangiwa na elimu duni juu ya umuhimu wa kutumia bima ya afya.

“Bima ya afya ni nzuri sana, lakini mtu anaona shida kwenda kulipa fedha taslimu atakazotumia kwa mwaka kwa ajili ya afya yake, lakini akiumwa atakwenda kununua dawa kwa zaidi ya fedha alizokataa kujiunga na bima ya afya, dawa zinapanda kutokana na masuala ya kiuchumi hivyo lazima tutafute mambo yatakayotupunguzia makali,” alisema.

Bila kuhusisha ripoti hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alisema kwa uhalisia mwananchi anapokwenda hospitali hutumia gharama nyingi, lakini akijiunga na bima ya afya hawezi kuziona gharama hizo.

“Mfano mgonjwa mwenye uhitaji wa kipimo cha CT Scan gharama yake inaweza kuwa Sh200,000, kama una bima ya afya huwezi kuiona gharama hiyo kwa sababu kupitia bima ya afya watu wengi wanachangia, kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo na presha Sh340,000 kwa mwaka ni kiwango kidogo sana,” alisema.

Januari 23, 2023 akizungumza na vyombo vya habari, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema changamoto kubwa ya wananchi katika kupata huduma za afya ni gharama.

“Bima ya afya ni kwa ajili ya kumsaidia Mtanzania, hususan maskini, mtu akipata mgonjwa atauza baiskeli yake, shamba lake, tuna kesi nyingi Watanzania wanauza mali zao ili kuwauguza wagonjwa, Serikali tumeona Bima ya Afya kwa wote ni moyo wa kumkomboa mwananchi kupata huduma bila kikwazo cha fedha.”

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernad Konga alisema kwa mwaka 2020/21 kumekuwa na ongezeko la watu wanaojiunga na bima ya afya kwa hiari, lakini katika kila Sh100 wanayochangia wanatumia zaidi ya Sh200.

“Mwaka 2020 walitumia huduma ya wastani kati ya asilimia 212 na mwaka 2021 walitumia huduma kwa asilimia 369, matokeo yake hawa wanaoingia kwa ulazima ndio wanabeba kundi kubwa,” alisema.

Kusubiri matibabu ni tatizo

Wakati ripoti ikionyesha ongezeko la matumizi ya kaya kwenye gharama za matibabu, suala jingine lililotajwa ni kusubiri huduma kwa muda mrefu.

“Wengi waliripoti kusubiri kwa muda mrefu kwenye vituo vya afya kama tatizo kubwa wanalokabiliana nalo wakati wa kutafuta matibabu,” ilinukuu ripoti hiyo.

Akizungumzia wagonjwa kusubiri muda mrefu, Mtaalamu wa Maabara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Alex Mlwisa, alisema kuwepo kwa wagonjwa wengi katika hospitali kuliko vifaa vya kutolea huduma ni kweli linachangia ongezeko la gharama kwa wagonjwa.

Mwaka 2022/23 bajeti ya Wizara ya Afya iliidhinishiwa Sh1.109 trilioni, kati ya fedha hizo, Sh200 bilioni ni kwa ajili ya vifaatiba, vitendanishi na ununuzi wa dawa. Kwa takwimu za Wizara ya Afya, Serikali inatoa Sh20 bilioni kila mwezi kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa dawa na hadi Desemba 2022 hali ya upatikanaji dawa ilikuwa asilimia 67 kutoka asilimia 62 Agosti 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live