Sakata la ununuzi wa Kampuni Tanga Cement limechukua sura mpya baada ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Profesa Edward Hoseah, kuipongeza Mahakama ya Ushindani (FCT) kwa kusitisha mchakato wa ununuzi wa kiwanda hicho huku akizitaka pande zote kuheshimu uamuzi wa mahakama hiyo.
Ununuzi wa kiwanda hicho licha ya kupatiwa baraka na Tume ya Ushindani (FCC), Oktoba 2021 kwa gharama ya Sh137 bilioni, Septemba 2022 FCT ilibatilisha baraka hizo.
Uamuzi wa FCC ungeipa kampuni ya Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement uwezo wa kununua asilimia 68.33 ya hisa za Tanga Cement baada ya kukubaliana na Kampuni ya Afrisam.
Akichangia maoni yake juu jana kuhusu uamuzi wa FCT, Profesa Hoseah alisema,“kwa maoni yangu, uamuzi wa Septemba 23, 2022 wa FCT yaliyoongozwa na Jaji Salma Maghimbi, lazima uheshimiwe kwa kuwa ulionyesha wazi uhitaji wa kuwalinda watumiaji wa huduma.”
Alisema Tanzania yenye uchumi wa chini wa kati, inahitaji sheria madhubuti kulinda uchumi wake dhidi ya ushindani usio wa haki.
“Najua ni kwa kiasi gani tunahitaji wawekezaji na Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akifanya kazi nzuri kuifungua Tanzania kwa wawekezaji,” alisema bosi huyo wa zamani wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Sakata la Kampuni ya Tanga Cement lilianza Oktoba 2021, wakati Scancem International DA (Scancem) – kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement – na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement, ilipotoa taarifa ya pamoja kuwa wamekamilisha masharti ambayo awali angepata asilimia 68.33 ya hisa katika kampuni ya Tanga Cement.
FCC tayari iliidhinisha mapendekezo ya ununuzi wa kampuni hiyo kwa Sh137.33 bilioni lakini kwa tahadhari kwamba kampuni itakayonunua Tanga cement isikifunge kiwanda hicho na iendelee kuzalisha na kuitangaza chapa ya Simba Cement (Tanga Cement) na isiwaachishe kazi wafanyakazi waliokuwepo.
Ni kutokana na sababu hizo, Kampuni ya Chalinze Cement Limited na Chama cha Watetezi wa Watumiaji Tanzania (TCAS) walikata rufaa FCT, ambayo ilitengua muungano huo uliopingwa kupitia hukumu iliyotolewa Septemba 23, 2022.
Hata hivyo, kutokana na muungano huo, baadhi ya wadau walipinga uamuzi kwa kile walichoeleza kuruhusu kuziunganisha kampuni ni kuvuruga ushindani. Mbali na kuvurugu ushindani walisema jambo linalotendeka ni kinyume cha sheria ya ushindani ya mwaka 2003.
Kampuni ya Cement ya Chalinze na chama cha watetezi wa watumiaji Tanzania (TCAS) walikata rufaa FCT, ambayo ilitengua muunganisho huo uliopingwa kupitia hukumu yake iliyotolewa Septemba 23, 2022.