Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unaweza kuwa milionea kwa kufuga funza

68572 Pic+funza

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa wengi wanaposikia neno funza, lazima miili iwasisimke. Hawakosei kwa kuwa ndiyo ukweli, kwa kuwa mdudu huyu ananasibishwa na uchafu ambao watu wengi hawaupendi.

Hata hivyo, wasichokijua watu hawa ni kuwa pamoja na uchafu wake, unaweza ukawekeza kwa mdudu huyu na hatimaye akakufanya kuwa na kipato kizuri maishani.

Iko hivi; unaweza ukawafuga funza kwa utaalamu na kisha kuifanya kazi hiyo kuwa biashara yako ya kukuingizia fedha. Na kama utaamua kuwekeza barabara, kwa nini usiwe milionea wa funza?

Kama ulikuwa hujui, tambua kuanzia leo kuwa wenzako tena wakiwamo wasomi, funza sio kinyaa kwao. Wengine wameweka kando vyeti vyao vya chuo kikuu na sasa wanafuga funza kwa mrengo wa biashara.

Hadithi ya Ibrahim Tajiri

Ibrahim Tajiri ni mmoja kati ya vijana walioamua kuchangamkia fursa ya ufugaji wa funza licha ya kuwa na shahaha ya uhasibu iliyo na wigo mkubwa wa ajira ndani na nje ya nchi. “ Niliamua kufuga funza kibiashara baada ya kufanya utafiti wangu mdogo na kubaini kuwa asilimia kubwa ya jiji la Dar es Salaam lina uchafu katika maeneo ya masoko, mitaroni, katika madampo na hata katika baadhi ya migahawa na hoteli. Niliamini ufugaji huu utasaidia kuondoa uchafu katika maeneo haya,’’ anasema.

Pia Soma

Kutoka hapo akaungana na wenzake walioamua kumtumia mdudu funza kama fursa ya biashara, kwa kuwa ni rahisi upatikanaji wake.

‘’ Funza hupenda kuzaliana katika maeneo yenye mlundikano wa uchafu na shombo za wanyama, samaki, mbogamboga na matunda, anaeleza Tajiri ambaye kwa sasa ameshakuwa mkufunzi wa ufugaji huo huku akitoa mafunzo kwa watu mbalimbali wanaohitaji kufuga funza.

Anasema kuna ana kuu mbili za funza, ambazo ni funza watokanao na inzi na funza wanaoleta madhara kwa viumbe hai kwa kuwasababisha magonjwa mbalimbali yakiwamo ya kutoboa miguu hasa kwa binadamu.

Faida za funza

Amana Msomaye ni mwanachama wa kikundi cha ufugaji wa funza na sungura kutoka Kibaha anasema biashara ya funza ni fursa, kwani ni rafiki kwa maendeleo na ana kiwango kikubwa cha viinilishe ambavyo ni muhimu kwa mifugo na wanyama mbalimbali.

“Tafiti nyingi zilizowahi kufanyika na nyingine zinazoendelea kufanyika zinaonyesha kuwa hapo baadaye funza anaweza kutumika kama chanzo cha protini badala ya samaki na soya” anasema.

Pia anasema funza wanaweza kutumika kama tiba kwa watu wenye vidonda. Kinachofanyika ni kupandikiza funza kwenye kidonda kwa minajili ya kula uozo uliopo na hivyo kuwa chachu ya kidonda kupona.

Mfugaji mwingine, Rehema Mwache anasema funza anaweza kutumiwa maabara kwa ajili ya kuua bakteria wa aina tofauti.

Ufugaji wake unavyofanyika

Tajiri anasema kuna aina tatu za uzalishaji wa funza; njia ya kwanza ni ya uzalishaji wa kawaida ambao hutumia ndoo au beseni kwa mfugaji kujaza uchafu wa aina mbalimbali na kufunika upande na kuacha nafasi ndogo kwa ajili ya inzi kuingia.

“Baada ya kuandaa hivyo, inzi lazima atakimbilia hapo kwa sababu anapenda vitu vyenye shombo na hivyo huanza kutaga mayai na baada ya saa 24 mayai hayo huanguliwa na baada ya siku tatu hadi tano, funza wanakuwa tayari wakubwa kwa matumizi ”anasema Tajiri

Baada ya kuwavuna, mfugaji atalazimika kumwagia maji ya uvuguvugu katika beseni au ndoo. Funza hao watakuwa wakielea juu, na hapo atawatoa na kisha kuwakausha juani.

Njia ya pili ya kufuga funza ni kutumia pumba za mahindi kwa kuziloanisha na kuzifunika kwa kutumia mfuko wa nailoni au gunia na kisha kuziweka katika chombo na baada ya siku tatu, funza wanakuwa tayari wameshazaliana.

Njia ya tatu, anasema: “ Hii ni njia ya kisasa na ya kibiashara zaidi. Hapa wazalishaji hutumia vizimba maalumu vya kufugia ambavyo vinapatikana katika ofisi za Mtandao wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita).

Tajiri anasema uzalishaji wa funza unachukua siku saba hadi 10 kabla ya kuwa tayari kwa ajili ya kuvunwa.

Chakula kwa mifugo

Matumizi ya funza

Mfugaji wa funza Mariam Msuya, anasema funza hutumiwa kama malisho ya mifugo kwa sababu wana kiwango kikubwa cha protini ambacho ni asilimia 60. Kiwango hiki ni kikubwa zaidi ya kile kinachopatikana katika dagaa na soya.

“Unajua kwenye soya kuna protini kwa asilimia 40 na kwenye dagaa kuna protini kwa asilimia 52, hivyo kama unafuga funza kwa ajili ya chakula cha mifugo, unakuwa katika nafasi nzuri ya kupunguza gharama za kununua chakula cha mifugo,” anaeleza.

Anasema Afrika Kusini inazalisha kwa wingi funza wanaotumika kama chakula cha mifugo hasa kuku, huku kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda inaongoza.

“Nchi zilizoendelea kama Afrika Kusini, hukamua funza na kupata mafuta ambayo hutumika katika shughuli mbalimbali zikiwamo za viwandani. Wanapokamuliwa, mabaki ndiyo yanayotumika kutengenezea chakula cha mifugo, anasema Tajiri.

Wasemavyo wataalamu

Neema Joshua ni mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe(TFNC). Anasema Watanzania hawatumii funza hivyo sio rahisi kwa mdudu huyo kutumika kama chakula, japo anaweza kuliwa na asilete madhara.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Ukiriguru mkoani Mwanza Paul Saidia, anasema watu wakibadilisha mtazano wanaweza kutumia funza kama chakula, kwani kuna baadhi ya maeneo watu wanakula funza ambao wanapatikana katika miti.

Soko la funza

Tajiri anasema kwa kupitia mtandao wao wameshapata soko hasa kutoka kwa watengenezaji wa vyakula vya mifugo.

“Lengo letu ni kuwauzia watengenezaji wa vyakula vya mifugo kwa gharama nafuu, ili waokoe fedha ambazo walikuwa wanatumia kwa ajili ya kununulia vyakula kutoka nje ya nchi ” anasema.

Anatoa wito kwa Watanzania kutumia mtandao wao au wataalamu wengine kwa minajili ya kujifunza ufugaji wa funza kitaalamu. Anasema funza hawafugwi kwa kukurupuka bali kwa utaratibu maalumu unaotokana na mafunzo kutoka kwa wataalamu wa ufugaji huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz