Baadhi ya Wakazi wa Mkoa wa Kagera wameliomba shirika la umeme nchini TANESCO kuwezesha kuwepo kwa umeme wa uhakika, ili kuwaondolea adha ya umeme kukatika hovyo, hali inayowasababishia hasara hasa kwa wale ambao wanategemea nishati hiyo katika uzalishaji. wakazi hao wamesema kuwa tatizo la kukatika kwa umeme linachangia kuchelewesha maendeleo yao na mkoa kwa ujumla, kutokana na kuharibu ratiba za uzalishaji mali, na mfumo mzima wa kufanya biashara.
"Umeme usiwe unazimika mara kwa mara, maana wakati mwingine inatokea muda huo unashughuli nyingi zinazohitaji umeme ndipo unazimika, hili ni tatizo kubwa kwetu maana linatusababishia hasara" wamesema wananchi wa Bukoba
Afisa uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Kagera, Samwel Mandari amesema kuwa moja ya changamoto zinazolikabili shirika hilo ni hujuma kwa miundombinu ya umeme, ikiwamo wizi wa nyaya kwenye transfoma na uchomaji wa moto katika misitu au mashamba, ambao husababisha nguzo kuungua, na kusababisha wananchi kukosa umeme.
"Sasa hivi shirika tunapenda kuwatangazia wananchi kwamba tumeanzisha kampeni maalumu ambayo tunavishirikisha vyombo vya dola ikiwamo polisi na taasisi nyingine za kisheria, kuwasaka watu wote wanaohusika na vitendo vya wizi wa nyaya na uchomaji nguzo moto, watakaobainika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi, niwaombe wananchi tutoe ushirikiano kwa hili" amesema Mandari.