Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umeme gridi ya taifa kichocheo uwekezaji migodi nchini

65293b673134baefb92c366a37521b94.PNG Umeme gridi ya taifa kichocheo uwekezaji migodi nchini

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefungua ukurasa mpya katika uwekezaji wa ndani kutokana na kutarajia kupata Sh bilioni 60 kwa kila mwaka kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Kiasi hicho kinatokana na kuuzia umeme mgodi huo mradi wa kuunganishia umeme wa Gridi ya Taifa utakapokamilika na kuanza kutoa huduma. Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande alieleza hayo hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba wa kuingia makubaliano hayo (Energy Supply Agreement) kati ya shirika hilo na GGML.

Makubaliano hayo yalifanyika Februari 21 mgodini hapo wilayani na mkoani Geita. Chande anabainisha mafanikio ya mkataba huo ni pamoja na kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na utaiwezesha Tanesco kuingiza Sh bilioni tano kila mwezi sawa na Sh bilioni 60 kwa mwaka kutokana na mauzo ya umeme katika mgodi huo. Mafanikio hayo yanajibu ombi la miaka 20 la mgodi huo kupatiwa huduma hiyo.

Kwa sasa mgodi huo utapata huduma ya umeme wa uhakika kutoka gridi ya taifa na kuuwezesha kuchangia zaidi pato la taifa. Hatua hiyo inazinufaisha pande zote mbili na kufungua ukurasa mpya kwa wawekezaji wa viwanda vikubwa na vya kati kwa Kanda ya Ziwa.

Makamu wa Rais wa Anglo- Gold Ashanti wanaomiliki mgodi wa GGML, Simon Shayo, akizungumzia manufaa ya mkataba huo kwa upande wao, alisema itapunguza athari za mazingira kwani kwa sasa matumizi ya mafuta mazito huchangia uharibifu wa mazingira na mgodi kulazimika kutumia gharama kubwa kukidhi kiwango bora cha uhifadhi mazingira. Pamoja na GGML kufanya vizuri na kupata tuzo mara kadhaa za uhifadhi wa mazingira kwa kiwango cha kitaifa na kimataifa bado ndoto na kiu yao ni kuona wanafanya kazi ya uwekezaji katika mazingira rafiki na yanayoendana na mabadiliko ya tabianchi ya nishati ya kijani (green energy).

“Kulinda mazingira ni jukumu na wajibu wetu kwanza na kisha mafanikio ni lazima kuanzia sisi tuwe mstari wa mbele katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kupitia mgodi wenyewe kwa manufaa na faida ya vizazi vijavyo,” anasema Shayo. Anasema walisubiri kwa muda mrefu hatua hiyo na sasa jukumu lao kubwa ni kupata mkandarasi wa kujenga kituo cha kupoozea umeme mgodini hapo yaani Sub Station Power, mchakato ambao tayari umefanyika.

Naye Mhandisi Mkuu wa GGML, Maftah Seif, anasema kwa sasa mgodi hutumia zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji mitambo pekee ambapo ni kununua mafuta mazito hivyo mkataba huo utaokoa mabilioni ya fedha kwa mwaka.

Maftah ameongeza kuwa kwa sasa GGML huzalisha kilovoti moja ya umeme kwa gharama ya Dola za Marekani senti 19 sawa na Sh 439.66 za Kitanzania hivyo baada ya mradi huo kukamilika mgodi utapata umeme kutoka Tanesco kwa gharama ya Dola za Marekani senti tisa sawa na Sh 208.26 kwa kilovoti moja kukiwa na unafuu mkubwa wa gharama. (Gharama hizo ni kwa ulinganisho wa thamani iliyokuwepo siku mkataba uliposainiwa).

Seif anasema watakapoanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa mgodini hapo, mbali na kupunguza gharama ya uendeshaji wa mitambo ikilinganishwa na jenereta lakini pia utaondoa tabaka la wimbi la uchafuzi wa mazingira hewani.

Meneja wa mradi wa kupeleka na kuunganisha huduma ya umeme katika mgodi huo kutoka Tanesco, Dismas Massawe, anasema kuwa baadhi ya masharti katika mkataba huo ni kuwa GGML akiwa mteja haruhusiwi kuzalisha umeme kwa mitambo yake yaani jenereta mgodini hapo isipokuwa kwa dharura tu kama itatokea.

Massawe ambaye ndiye anayeongoza timu ya kutekeleza mradi huo wa kupeleka umeme mgodini humo, Tanesco imejipanga kuhakikisha kazi hiyo inamalizika ifikapo Agosti mwaka huu kwa kuweka nguzo pamoja na miundombinu ya kusafirisha umeme. Anasema kazi hiyo inafanywa kwa usimamizi wa wataalamu mahiri wa Tanesco ambapo mkandarasi anayefanya kazi ya kuweka na kujenga miundombinu ya usafirishaji ni kampuni ya China ya CAMC Engineering Company Ltd huku mkandarasi anayefanyakazi ya kujenga na kuweka miundombinu ya kusambaza umeme ni Kampuni ya Steg International Services kutoka nchini Tunisia.

Massawe anasema kuwa lengo la serikali kupitia Tanesco ni kuweka miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme katika migodi yote nchini ikiwemo ya wachimbaji wadogo na wa kati ili kuhakikisha wanafikiwa na huduma hiyo kwa maslahi ya mwekezaji mhusika na taifa. Anasema kuwa migodi mingine ya dhahabu mikubwa iliyopo Kanda ya Ziwa ikiwemo Nyamongo uliopo mkoani Mara, Bulyan’hulu na Buzwagi iliyopo wilayani Kahama, inatumia huduma ya nishati ya umeme wa Tanesco.

Anasema hatua hiyo inatoa fursa kwa mgodi unaotarajiwa kujengwa na Kampuni ya Tanzos Mining katika Kijiji cha Imwelu, Kata ya Buseresere, wilayani Chato, mkoani Meneja wa Mradi wa Kupeleka Umeme wa Tanesco mgodi wa GGML, Dismas Massawe (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande (katikati) baada ya kusainiwa kwa mkataba wa kuuziana umeme kati ya Tanesco na GGML mgodini hapo. Geita utakaounganishwa na umeme hatua itakayouwezesha kuendeshwa kwa umeme wa Tanesco wa gharama nafuu zaidi ya jenereta.

Mgodi wa kati uliopo kijijini Busolwa, Kata ya Nyarugusu, wilayani Geita wa Busolwa unaoamilikiwa na mwekezaji mzawa, Baraka Nyandu ni miongoni mwa migodi inayoingiza mapato Tanesco kutokana na kutumia umeme wake na kuachana na matumizi ya jenereta. Hata hivyo, mgodi huo unadai ulitumia gharama kubwa kuvuta umeme huo.

Massawe anasema mradi huo wa thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 23 sawa na Sh bilioni 52.9 utapeleka umeme wenye msongo wa KV33 kwa umbali kilometa sita na Tanesco itakamilisha kazi hiyo Agosti mwaka huu wakati GGML wao watakamilisha Desemba.

Kituo cha kupoozea umeme cha Mponvu kitakuwa na uwezo wa kuchakata megawati 792 lakini kwa sasa kitaanza kwa kuchakata megawati 90 na katika megawati hizo mgodi wa GGML mahitaji yake ni megawati 40.

Anasema wateja wengine wa mkoa huo wanatumia megawati 16 tu hivyo megawati 34 zitakazobaki kama ziada zitatumika kusambazwa kwa wahitaji wengine wakiwemo wawekezaji na wachimbaji wadogo wakiwemo wanaomiliki viwanda vidogo vya kuchakata dhahabu vikiwemo Ellutions na Plants. Meneja wa Tanesco Mkoa wa Geita, Joachim Rueta anasema mradi huo unakwenda sambamba na kuunganishwa umeme katika vijiji 129 kati ya vijiji 474 vya Mkoa wa Geita vinavyotakiwa kuunganishiwa umeme kabla ya Desemba mwaka huu.

Rueta anaongeza kuwa vijiji 57 kati ya vijiji hivyo 129 ambavyo havijaunganishiwa huduma ya umeme, wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu kwani vipo katika mpango wa utekelezaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya tatu mzunguko wa pili utakaokamilika Desemba 2022. Anasema serikali kupitia Tanesco inajitahidi kuhakikisha Watanzania kote nchini wanafikiwa na huduma hiyo ili kuchagiza kupatikana kwa maendeleo kwa haraka. Mwandishi ni mchangiaji wa makala wa gazeti hili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live