Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wavuvi kuchangamkia fursa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ya ugawaji wa maboti na vizimba ili waweze kufanya shughuli zao kisasa na kuboresha maisha yao.
Waziri Ulega ametoa rai hiyo alipofanya ziara katika Soko la Samaki la Kimataifa la Kilumba alipowatembelea wavuvi hao Leo Oktoba 4, 2023 kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wavuvi hao mkoani Mwanza.
Alisema fursa hiyo ya vifaa vya kisasa aliyoitoa Rais Samia wakiitumia vizuri na wakafanya uvuvi na ufugaji wa kisasa wa samaki aina ya sato itasaidia ziwa victoria kupumua na itapelekea samaki aina ya sangara na dagaa kuongezeka na kuinua uchumi wao.
"Tutumie fursa hiyo vizuri, tuzalishe vya kutosha ili Mhe. Rais aone umuhimu wa kutuongeza vyombo vingine vya kisasa kwa sababu yeye anachokifanya ni kutuwekea mazingira mazuri ili tuendelee kunufaika na shughuli zetu", alisema Mhe. Ulega
Kuhusu kero za tozo, Waziri Ulega amewataka wavuvi hao kuwa na subira wakati jambo hilo linaendelea kufanywa kazi na mamlaka husika.
Aidha, alimuelekeza Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Stephen Lukanga kuhakikisha anaweka mikakati madhubuti ya kukomesha uvuvi haramu na kuhakikisha biashara ya mazao ya uvuvi inafanyika katika masoko rasmi huku akimpa mwezi mmoja kutekeleza maagizo hayo.