Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira mazuri kupitia fursa za Utalii wa Bahari ili wavuvi hasa wadogo waweze kunufaika kwa kuuza samaki na mazao yake.
Waziri Ulega alisema hayo wakati wa tukio la mashindano ya Ngalawa (Ngalawa race) lililofanyika kwenye ufukwe wa Kendwa uliopo Mkoa wa Kaskazini Unguja Juni 22, 2023.
Alisema kuwa kupitia mashindano hayo shughuli za uvuvi zitatangazika duniani na kuvuta watalii wengi na hivyo wavuvi watapata fursa nzuri ya kufanya biashara ya samaki.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yanachagiza ujio wa watalii nchini na hivyo kupelekea utalii wa bahari kushamiri kitendo ambacho kinaongeza fursa ya biashara kwa wavuvi.
"Tunataka huu utalii wa bahari uwanufaishe moja kwa moja wavuvi wadogo waweze kupata kipato chao kutokana na mauzo ya samaki na mazao yake kwa watalii hao," alisema.
Aidha, Ulega aliwashauri wavuvi kutumia vyema mwambao wa Bahari kwa kuanza kufanya shughuli mbadala za kujiongezea kipato ikiwemo ufugaji wa Kaa, Kambakochi na Majongoo Bahari.
Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuwainua wavuvi na ndio maana inafanya kila jitihada za kuboresha shughuli zao ili ziwe na mchango mkubwa na thamani yake ionekane kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.